Chombezo : Mwajuma Utamu Sehemu Ya Mwisho
Nilichokisikia wakati
nilipokuwa nimefumba macho yangu ni milio ya risasi, niliamini risasi hizo
nilipigwa mimi, nilipoyafungua macho yangu kwa mara nyingine sikutaka kuamini
kile nilichokuwa nikikishuhudia. Niliuona mwili wa Damian ukiwa chini huku
ukitapatapa, damu zilikuwa zikimtoka kutokana na risasi alizokuwa amepigwa.
Ghafla! niliwaona polisi wakiwa ndani ya chumba hicho, sikutaka kuamini kile
kilichokuwa kimetokea katika maisha yangu, yaani kama sio kutokea polisi
ningeshakuwa maiti siku nyingi.
Polisi walinisaidia kunifungua kamba nilizokuwa nimefungwa nazo miguuni na
mikononi, siku hiyo ndiyo ilikuwa mwanzo wa kuokoka na kifo nilichokuwa
nimekikaribia.
Polisi walionekana kufanikiwa kazi yao kwa asilimia mia moja kwani muuaji huyo
aliwasumbua mno, siku hiyo ndiyo walifanikiwa kumkamata na baada ya kumpiga
risasi alifariki dunia hapohapo.
****
Baada ya kunisurika kifo na Damian au jini mweusi kama alivyokuwa akijulikana
niliachana na biashara ya uchangudoa, sio mimi tu bali hata Suzie na yeye
alichana na biashara hiyo.
Jambo la kushangaza baada ya Martin kurudi kutoka Dubai, Suzie aliitumia nafasi
hiyo kumueleza kila kitu ambacho kilitokea katika maisha yangu.
Martin alinichukia baada ya kuambiwa hayo na kama haitoshi aliamua kuhamisha
mapenzi kwa Suzie ambapo walifanikiwa kufunga ndoa na kubahatika kuzaa watoto
mapacha, Gracious na Precious.
Niliumia sana baada ya tukio hilo kutokea hata hivyo sikuwa na wa kumlaumu,
maisha yangu niliyachezea mwenyewe.
Baada ya kupita miezi mitatu niliamua kwenda kupima, majibu yalionyesha kuwa
nilipata maambukizi ya virusi vya ukimwi hivyo nilitakiwa kuanza kutumia
vidonge vya ARV kwa ajili ya kuongeza siku za kuishi.
Ni pigo kubwa katika maisha yangu, kiukweli najutia mambo mengi tena machafu
niliyoyafanya katika maisha yangu, idadi ya wanaume niliyotembea nao inafika
mia tatu.
Maisha ya mjini yalinishinda, niliuza kila kitu nilichoachiwa na Martin kama
zawadi katika maisha yangu. Japokuwa ni miaka mingi sana imepita tangu
nilipoondoka nyumbani kwetu Mtwara lakini niliamua kurudi.
Sikuwa ni Mwajuma yule wa zamani tena ambaye nilionekana kuwa mrembo wa sura
mpaka umbo la kumvutia mwanaume yoyoye rijali, huyu wa sasa nilikuwa naishi na
virusi vya ukimwi na muda wowote Mungu anaweza kunichukua kwani afya yangu
imezidi kudhoofika.
FUNZO: Katika maisha wakati mwingine jifunze kutokana na makosa ya mtu mwingine,
nimeamua kukusimulia kumbukumbu za maisha yangu ili na wewe ujifunze kutokana
na makosa niliyoyafanya.
Naomba ukimaliza kuisoma kumbukumbu hii uyachukue yale yote mazuri kisha
uyafanyie kazi na yale yote mabaya tafadhali naomba usiyachukue. Narudia tena
katika maisha wakati mwingine jifunze kutokana na makosa aliyoyafanya mtu
mwingine.
MWISHO.