KARIBU USOME HADITHI NZURI ZA KUSISIMUA

Chombezo : Utamu Wa Shemeji Flora Sehemu Ya Ishirini na Tano (25)

SIMULIZI NZURI YA KUSISIMUA
Kwa kuwa kifo cha Lukasi na mkewe Flora kilikuwa kimeleta taharuki kwa familia zote mbili yaani familia ya akina Lukasi pamoja na ya mkewe Flora. Hivyo ndugu na jamaa wa upande wa akina Flora nao baada ya kukamilisha mazishi waliweza kuja mpaka kijijini nyumbani kwa akina Japhet wakiamini hapa labda wanaweza kuupata ukweli wote juu ya vifo vya wanandoa hao. Ukizingatia Japhet ndio mtu pekee ambaye ndie alikuwa anaishi nyumba moja na marehemu hao kabla hawajafariki dunia.

Kikao cha kifamilia kiliweza kuitishwa Mara moja na Japhet akawekwa mtu kati apate kutoa maelezo ya nini kilitokea.

"Hayaa Japhet kijana wetu tunajua kama wewe ndie ndugu pekee uliyekuwa unaishi pamoja na marehemu kaka yako na Shemeji yako, hivyo tunaomba hapa utuambie nini kimesababisha mpaka ugomvi ukaweza kutokea na kaka yako akamuua mkewe na halafu yeye pia kujiua?" Mjomba wa Japhet aliyepewa dhamana ya kuendesha kikao hicho alianza kumchachafya Japhet. 

Kwa upande wa Japhet mwenyewe hakujua hata aeleze nini hapa kwa wanandugu ili apate kueleweka mwisho akaamua kujitetea. "Ni sawa inajulikana hivyo kuwa nilikuwa naishi nyumba moja na marehemu kaka pamoja na Shemeji, lakini mimi siku za hivi karibuni nilikuwa nimehama nyumbani kwao nina maisha yangu ya kujitegemea" Japhet alisema ili kujivua na msala huo. 

Baba yake Japhet akaingilia kati: "Hilo la kusema umehama nyumbani kwa kaka yako sisi hatulijui kabisa, tunachojua wewe ulikuwa unaishi na kaka yako tuambie nini kilitokea?" Baba yake Japhet alisema na watu wote wakamuunga mkono kumsapoti.

"Lakini baba mimi sijui nini chanzo cha ugomvi wa kaka na Shemeji mpaka wakafikia hatua ya kuuana" Japhet alisema. Mjomba wake naye akauliza:

"Sasa nani anajua hicho chanzo cha ugomvi wao?" Mjomba aliuliza. Japhet akajifikiria kidogo halafu akasema: "Mimi pia sijui labda mwenye majibu hayo ni yule binti aliyekuwa anawasaidia kufanya kazi za ndani" Japhet alisema. Wanandugu wakabaki wanajidaliana pale kidogo halafu mjomba wake na Japhet akauliza tena: "Sawa tumepata taharifa za huyo binti kuwa anashikiliwa kituo cha Polisi kwa mahojiano zaidi, lakini pia kesho tutaenda wote mpaka huko mjini pamoja na wewe hadi kituoni ili kujua huyo binti amesema nini kwa maaskari pia tunaomba utuambie ni kwanini ulihama nyumbani kwa kaka yako?" 

Mjomba wake alimuuliza Japhet na watu wote kwenye hicho kikao cha kifamilia walikuwa wanasubiri kujua nini sababu ya Japhet kuhama ghafla nyumbani kwa marehemu kaka yake na Shemeji yake.

Japhet hapo alibakia ameduwaa na kujiuliza ataanzaje kusema ukweli kuwa eti alihama kumkimbia Shemeji yake Flora aliyekuwa anamsumbua kwa kumtaka kimapenzi? Hilo Japhet akaona haliwezekani kusema mbele ya familia.

Japhet akabakia kimya anakuna kichwa.

"Tunasubiri jibu lako Japhet, tuambie ni kwanini ulihama nyumbani kwa kaka yako?" Mjomba alizidi kumkomalia.

"Mimi niliamua kuhama nyumbani kwa kaka pamoja na Shemeji, ili niende nikaanze maisha yangu ya kujitegemea na sio vinginevyo" Japhet alijbu kwa kujiamini. "Ok basi hakuna shida maelezo yote tutaenda kuyajua hiyo kesho baada ya kufika mjini ndio tutajua na huyo binti ameeleza nini huko kituoni" Mjomba alisema na kikao kikaweza kufungwa.

Japhet licha ya kujitetea hapa mbele ya wanandugu na kujisafisha asionekane kama yeye ndio chanzo cha ugomvi wa marehemu kaka yake na mkewe Flora baada ya kuwahisi wana mahusiano ya kimapenzi. Hofu yake Japhet ilikuwa ni kwa Rozi huko kituoni anaposhikiliwa endapo kama atakuwa amewaambia ukweli maaskari juu ya tukio lilivyokuwa.

Japhet alizidi kuchoka baada ya kugundua na yeye pia atatakiwa kutoa maelezo yatakayofanana na maelezo ya Rozi ili kuondoa utata juu ya kifo cha kaka yake pamoja na Shemeji yake Flora ambao ugomvi wao mpaka uliopelekea vifo ukidaiwa ni wivu wa kimapenzi.

Kijana Japhet alijikuta anapagawa zaidi!.



Kijana Japhet alijikuta anapagawa zaidi.

Basi hakuwa na ujanja tena wa kufanya kitu chochote Kwani ndio vile lile wazo la kukimbia pale mwanzo alishalikataa. Na sasa alichokuwa anakisubiri ni kurudi tu mjini na kwenda kuripoti kituo cha Polisi kama alivyotakiwa na wale maaskari waliokuja kufanya uchunguzi kule mjini nyumbani kwa marehemu kaka yake Lukasi wakati alipomuua mkewe Flora na halafu pia na yeye kujiua. 

Usiku ukaweza nao kuingia baada ya shughuli na pilika za msiba zote kukamilika waombolezaji wakalala wakisubiri asubuhi ya siku inayofuatia waanze safari ya kurudi tena Dar es salaam Kwani kama ni shughuli ya mazishi iliyowaleta Dodoma kumzika Lukasi pamoja na mkewe Flora walikuwa wameshaimaliza. Japhet usiku huo hakuweza kupata usingizi wa kueleweka mawazo yake yote alikuwa anafikiria ni jinsi gani atakapofika mjini atavyotoa maelezo yake mbele ya Askari Polisi.

"Sitakiwi kuwa na uoga kupita kiasi kama ingekuwa ni tatizo sana basi na mimi pia wangenikamata kama walivyofanya kwa Rozi, na wasingeniruhusu kuja kuzika" Japhet alijisemea moyoni na kujifariji.

Basi akapitiwa na usingizi mzito akalala.

Asubuhi ya siku nyingine ikaweza kufika na baada ya kuamka zikafanyika taratibu nyingine ndogondogo za hapo nyumbani na baada ya hapo safari ya kurejea tena mjini Dar es salaam ikaanza huku ndugu muhimu nao wakiwemo kama vile wazazi wa Japhet baadhi ya ndugu wengine wao walibakia kijijini hapo wakimalizia msiba (Matanga) kama inavyotakiwa kimila.



Kwenye Majira ya jioni ndio waliweza kufika salama kabisa mjini Dar es salaam moja kwa moja safari ikahitimishwa pale pale nyumbani kwa marehemu Lukasi na Flora ambapo ndio palipotokea msiba.

Baada ya kufika hapo wakaingia ndani ya nyumba hiyo huku kila mmoja akiwa yupo na huzuni moyoni mwake akikumbuka wahusika wakuu wa nyumba (Lukasi na mkewe Flora) ndio hivyo hawapo tena hapa duniani. Kwa upande wa Japhet yeye maumivu ndio yalimzidi maradufu.

Basi baada ya hapo kama inavyokuwa marehemu akishazikwa na msiba tena nao ndio unahesabika umeisha. Hivyo ndugu na jamaa baadhi yao kila mmoja akaenda nyumbani kwake kupambana na maisha yake kwa ajili ya familia yake. Hapo kwenye nyumba ya nyumba ya Lukasi walibakia wazazi wa marehemu Lukasi pamoja na mjomba bila kumsahau na Japhet mwenyewe naye alikuwepo huku ndugu wa marehemu Flora alibakia kaka pamoja na dada yake (Flora) baada ya hapo kikaitishwa tena kikao kidogo cha kifamilia kujadili ni nani ambaye atakuwa anasimamia hapo nyumbani na kuangalia vitu vyote vilivyoachwa na hao wapendwa wao waliotoka kuwazika. 

Kwa kuwa Lukasi na Flora hawakubahatika kuwa na mtoto katika maisha yao yote ya ndoa basi Japhet akapendekezwa kuwa ndio atakuwa msimamizi mkuu wa Mali za marehemu kaka yake. Hakukuwa na aliyepinga wazo hilo wote wakakubaliana na maamuzi hayo. "Kesho asubuhi wote tutaenda huko kituoni kusikiliza kama Polisi wameweza kubaini chochote juu ya chanzo cha vifo vya ndugu zetu" Mjomba wa Japhet alisema. 

Japhet naye akapata muda wa kutafakari na kupanga ni jinsi gani ataenda kujibu maswali ya Polisi hao watakapokuwa wanamuhoji kituoni. Baada ya kuoga na kumaliza kula chakula wote wakaingia vyumbani kulala huku Japhet akienda kulala na kaka yake Flora kwenye kile chumba chake alichokuwa analala hapa kabla ya kuhama. Japhet alikumbuka mengi sana na kuwaza ni vipi ataweza kuishi bila ya kaka yake (Lukasi) Kwani ndio alikuwa ni tegemeo na msaada Mkubwa sana kwake.

 "Kweli nimepata pigo maishani kuondokewa na kaka yangu, naomba Mungu anisamehe kwa dhambi ya usaliti niliyoifanya na Shemeji yangu mpaka ikasababisha lile balaa" Japhet alijisemea moyoni kwa huzuni. "Nikifanikiwa kumaliza hili jambo salama, kuanzia kesho nitaenda kanisani na nitatubu dhambi zangu zote kwa Mungu na kuokoka kabisa!" Japhet alijiapiza ndani ya moyo wake. Ndio hivyo tena maji yakimwagika hayazoleki yote yaliyotokea ndio tayari yameshatokea yanabakia kuwa majuto ndani ya Nafsi.



Asubuhi ikafika na wote wakaamka Pole pamoja na rambirambi za majirani wa hapo mtaani walizidi kuzipokea kwa wingi. Muda wa kwenda kituoni ulipofika Japhet pamoja na baba yake na mjomba wake bila kumsahau na yule kaka wa Flora wakaingia kwenye gari ya mjomba wake na Japhet wakaanza safari ya kuelekea kituoni kusikiliza kama Rozi atakuwa amesema kitu chochote labda cha kuwasaidia kujua nini kilisababisha mpaka marehemu walikuwa na ugomvi mpaka kufikia hatua ya kuuana. 

Japhet japo alikuwa anajua kila kitu ambacho kilitokea lakini aliamua 'kupiga kimya' (Kunyamaza) mpaka atakapofika huko kituoni kusikiliza Rozi atakuwa ametoa maelezo gani. Baada ya kufika mpaka kituoni moja kwa moja wakaingia ofisini kwa Askari anayeshikilia kesi hiyo na baada ya kuonana na Askari huyo wakaanza mazungumzo rasmi. "Ndio Bwana Afande sisi tumerejea kutoka mazikoni, vipi yule binti ameweza kusema chanzo cha tukio?" Mjomba wa Japhet alimuuliza huyo Polisi.

"Kwanza nawapeni pole nyingi sana kwa kuondokewa na wapendwa wenu, hapa sisi kwa upande wetu tumeshindwa kujua nini chanzo kilichopekea mpaka wale wanandoa kuwa na ugomvi ambao ndio uliosababisha vifo vyao" Polisi huyo alitoa maelezo kwa kirefu sana. "Sawa je yule binti aliyekuwa anafanya kazi za ndani kule nyumbani kwao naye amesemaje?" Baba yake Japhet naye aliuliza.

"Kusema ukweli tangu yule binti tulipomchukua kwa ajili ya mahojiano naye amesema hajui kitu chochote juu ya ugomvi Kwani aliwasikia tu wanagombana na baadae yeye kufungiwa chumbani kwa ndani mpaka alipokuja kufunguliwa mlango na majirani" Polisi huyo alisema. 

Hapo kidogo hata Japhet akajikuta anapata afueni kwa kusikia hivyo. "Duuh siamini kama Rozi ameweza kuepusha hii kesi kwa kuficha siri" Japhet alijisemea moyoni na kumpongeza Rozi.

INAENDELEA
Powered by Blogger.