KARIBU USOME HADITHI NZURI ZA KUSISIMUA

Simulizi : Singidani Sehemu Ya Nne (4)

Simulizi ya singidani
Ni saa nne na dakika zake usiku. Chris alikuwa anatoka kwenye Baa ya G8, Kibaoni. Kutoka hapo hadi ilipo hoteli yake ni jirani mno, ni mwendo wa dakika mbili tu kwa miguu. Njiani akakutana na mmoja wa wahudumu wa hoteli aliyofikia.

Akamwambia: “Kaka unatafutwa na maaskari. Kumbe yule mwanamke uliyekuwa naye chumbani ni mke wa polisi, tena ni mkuu pale Central. Wamekuja maaskari wanne na silaha wanakutafuta. Mimi nakushauri usirudi tena. Tafuta mahali ulale mpaka asubuhi wakati tukitafuta ufumbuzi wa hili jambo,” alisema akionekana kujawa na wasiwasi mwingi.Pombe yote ilimruka!



I kama alikuwa hajanywa hata tone moja la pombe. Kichwa kilikuwa tupu kabisa. Bado alikuwa na maswali mengi kichwani mwake; inawezekana kweli Laura akawa mke wa mtu? Labda inawezekana lakini vipi amwache mumewe na kwenda kujirusha klabu?

Kichwa kiliwaka moto. Aliumizwa na mengi. Achana na kukamatwa na pengine kufunguliwa mashitaka lakini alijilaumu kwa kujichelewesha kumpata. Angalau angekuwa amefaidi uzuri wake, kidogo ingepooza maumivu ya kile alichoelekea kukikabilia.

Alimwangalia yule msichana kwa jicho lenye maswali lukuki, lakini alionekana kama ambaye hana majibu sahihi ya maswali yaliyozunguka kichwani mwake.

“Sikia dada, mimi huwa sipendi mizaha kabisa. Hebu niambie ukweli, kuna maaskari wamekuja pale?”

“Ndiyo!”

“Wamevaa nguo za polisi?”

“Ndiyo, tena kuna mwingine amevaa koti jeusi.”

Moyo wa Chis ukalipuka.

“Wamenitaja jina?”

“Ndiyo. Wamesema wanamtaka Dk. Chris. Tena alitaka tuwafungulie mlango ili wakague chumba chako, tukakataa. Kwa inavyoonekana itakuwa ni kweli. Hili ni tatizo kaka yangu, tafuta mahali pengine pa kulala.”

Chris akatulia kidogo.

Mawazo yakazidi kumwandama. Kuna kitu aliwaza; iweje leo hii Laura awe mke wa mtu? Mbona hakuwa na pete kidoleni? Laura si mwanafunzi?

“Au kuna mchezo nachezewa?” akajiuliza Chris.

“Halafu kama ni mchezo mtu wa kunisaidia hapa ni mmoja tu, Maulanga.”

Ni kweli Maulanga, dereva taksi aliyekuwa akimtumia kwa mizunguko yake pale mjini ndiye ambaye angeweza kumsaidia kujua ukweli wa tukio lile. Ni Maulanga huyohuyo ndiye aliyempeleka Laura kwenye nyumba anayoishi.

“Kwahiyo dada unanishauri nisije kabisa pale?”

“Huna haja ya kufanya hivyo, lakini kama unaona nakudanganya nenda. Wamesema watarudi tena baadaye, maana wameagizwa na mkuu wao, ukamatwe kabla ya asubuhi.”

Moyo wa Chris ukapiga.

“Sawa, ahsante kwa taarifa. Ngoja nitulize kichwa, nitajua cha kufanya. Kwa sasa naomba tu unisaidie namba yako ya simu tafadhali,” akasema Chris, yule dada akatekeleza.

“Unaitwa nani vile?”

“Mwanjaa.”

“Ok.”

Palepale Chris akaamua kubadilisha kiwanja ili atulize kichwa chake wakati akitafakari cha kufanya. Mwanjaa alirudi zake alipotoka, Chris akachukua bodaboda na kumwambia dereva ampeleke Baa ya Serengeti iliyokuwa katikati ya mji.

***

Chris akiwa Serengeti Bar, alimpigia simu Maulanga na kumwambia amfuate pale haraka sana. Maulanga hakuwa mbali na eneo, alikuwa ameegesha jirani na Benki ya CRDB, lilipo Jengo la TRA la Mkoa wa Singida. Dakika mbili baadaye alikuwa pale.

“Hivi yule msichana uliyempeleka hosteli jana usiku unamfahamu?”

“Namuona sana klabu karibu kila wikiendi, huwa anakuja na rafiki zake.”

“Unajua kuwa ni mke wa mtu?”

“Mke wa mtu? Sina hakika kwa kweli.”

“Kivipi?”

“Yaani sifahamu chochote ingawa nahisi kwamba atakuwa ni mwanafunzi. Si anasoma chuo?”

“Kwanini unasema unahisi? Kwani siku ile hukumfikisha hosteli?”

“Kuna nyumba aliingia, akasema anaishi hapo na dada yake.”

“Lakini mimi aliniambia anaishi hosteli. Dah! Sijui hii ishu ikoje! Nasikia wamekuja maaskari pale gesti, wananitafuta.. eti wanasema niliingia na mke wa mtu mle ndani na mumewe ni askari.”

“Mh! Mbona majanga haya kaka. Sasa unafanyaje?”

“Niachie mwenyewe, nitajua cha kufanya. Wewe nenda, nitakuita baadaye.”

“Poa.”

Chris alianza kunywa upya kabisa. Baadaye akapata wazo. Alitakiwa kupumzika ili siku inayofuata aweze kwenda zake kijijini kwao. Wazo la Laura alishalifuta kabisa. Aliona tatizo likiwa mbele yake waziwazi kabisa!

Akatoka pale Serengeti Bar na kutafuta gesti nyingine jirani na eneo lile, akalala. Katikati ya usiku, simu yake ikapigwa. Alipoangalia kwenye kioo cha simu, alishtuka sana.

Alikuwa ni Laura anampigia!


MACHO ya mshangao yalimtoka. Woga ukamjaa moyoni mwake. Alibaki akiingalia ile simu bila kuipokea. Mara simu ikakatika. Hapo sasa akapata nafasi ya kuangalia simu yake vizuri.

Alikuta meseji nne, zote zilitoka kwa Laura. Alipoifungua ya kwanza tu, simu ikaanza kuita tena. Chris akazidi kuogopa. Akili yake ilimtuma kwamba, huenda aliyekuwa akipiga alikuwa ni mume wa Laura au walikuwa pamoja na alilazimishwa kufanya hivyo ili aingie mtegoni.

Hakuwa tayari!

Simu ilipokatika, mara moja akaanza kusoma ile meseji. Maneno aliyoyasoma yalimchanganya sana. Hakuamini alichokiona. Meseji ile iliandikwa: “Kwa muda mfupi sana umeuteka moyo wangu, tafadhali Chris usinitese. Mbona hujanitafuta wakati tulikubaliana tukutane klabu?”

Inawezekana vipi mwanamke ambaye aliambiwa ni mke wa mtu ampigie simu usiku ule tena akimwambia kuwa anatakiwa kwenda kukutana naye klabu? Jambo hilo lilimchanganya sana kichwa chake.

Akaendelea kusoma nyingine mfululizo: “Baba vipi jamani? Mbona kimya? Acha kunitesa.”

“Chris nimekuwa tayari kukukabidhi moyo wangu wote kwako, mbona sasa huonyeshi kuwa upo tayari?”

“Sikia, tayari mimi nipo klabu hapa, kama huji niambie nirudi zangu hosteli nikapumzike. Nimekuja hapa kwa ajili yako Chris.”

Meseji ya mwisho ndiyo iliyomchanganya zaidi. Anamwambia anataka kwenda hosteli? Ni hosteli gani wakati alishaambiwa kuwa ni mke wa mtu?

Kwa hakika usingizi wote ulipotea. Pamoja na yote hayo, alijua alikuwa mtegoni na kama angejibu chochote angeweza kukamatwa mara moja. Kwa mtu mkubwa kama mkuu wa kituo cha polisi, maana yake ni kwamba, kama angeamua kumfanyia chochote kwa kosa la kutembea na mke wake, angeweza!

Wazo moja la haraka likamvamia kichwani mwake; alitakiwa kuvunja kabisa line yake. Hakutakiwa kupatikana tena kwa namba ile. Hilo ndilo wazo lililomwingia kwa kasi sana. Hakutaka kufikiria sana kuhusu hilo.

Akavunja ile line na kuitupilia mbali!

“Shiiit! Tuone sasa, watanipata wapi! Kwanza mimi sijafumaniwa. Najua wakiamua kunitafuta watanipata, lakini natakiwa kuwa mjanja sana kwenye eneo hilo. Hawawezi kunikamata asilani.”

Hasira ilimjaa moyoni. Alishindwa kuelewa ni kwa nini Laura aliamua kumdanganya kuwa hajaolewa wakati alikuwa mke wa mtu, tena wa askari kabisa. Jambo hilo lilimuumiza sana.

Akajilazimisha kulala.

***

Nani asiyemjua Dk. Chris, msanii wa filamu za Kibongo? Kila kona alijulikana. Hilo lilimaanisha kuwa, kama polisi mkoani Singida wangeamua kumtafuta kwa dhati kabisa, wangemkamata mapema sana asubuhi hiyo.

Chris alilijua hilo. Mara baada ya kuamka, alikwenda moja kwa moja mapokezi na kumuomba mhudumu akamnunulie kofia ya kapero. Yule mhudumu hakuwa na maswali mengi, alichukua fedha kwa Chris kisha akaenda kununua kofia na kumpelekea.

Chris akaichukua na kuivaa baada ya kujiandaa kikamilifu. Alitoka nje ya gesti hiyo na kutembea kwa mwendo wenye tahadhari zote. Taratibu akiwa ameuficha uso wake kwa kapero, alikodi teksi na kumtaka dereva ampeleke stendi kuu ya mabasi mkoani Singida, Misuna.

Dakika tano tu zilitosha kumfikisha kituoni hapo. Alishuka na kumlipa dereva kisha akatembea hadi katika ofisi za basi la Beffe, linalofanya safari zake kutoka mjini kwenda wilayani Mkalama kupitia Iguguno na Nduguti.

“Gari linaondoka saa ngapi?” Chris akamwuliza dada aliyekuwa akimkatia tiketi.

“Saa tano kamili, kwa sababu leo tunapita hadi Meatu.”

“Sawa, nipatie tiketi lakini kuna shughuli zangu nazifanya hapa mjini, sitapandia hapa. Mtanikuta kwenye mizani huo muda.”

“Tafadhali usije kulalamika umeachwa, saa tano juu ya alama uwe pale, sisi tutakukuta hapo.”

“Haina shida dada.”

Chris akalipa kisha akaondoka zake na kwenda kuchukua teksi nyingine iliyompeleka Kibaoni, ambapo ndipo gesti iliyokuwa na begi lake na vitu vyake vingine. Gari liliingia eneo hilo na kuegesha mbele ya geti.

“Naomba ukaniitie mhudumu tafadhali,” Chris akamwomba yule dereva ambaye alitii.

Sekunde chache sana, Mwanjaa alitokea, akakutana na swali kutoka kwa Chris: “Vipi, jamaa walirudi tena jana?”

Chris alisubiria jibu la Mwanjaa akiwa mwenye wasiwasi mwingi sana. Bado hakuijua hatma yake.



WASIWASI ulimjaa moyoni akiwa hajui kabisa kilichotokea usiku wa kuamkia siku hiyo. Macho yake aliyatuliza usoni mwa Mwanjaa akisubiri kusikia jibu lake. Mwanjaa alionekana kusita kidogo.

“Vipi... walikuja? Naomba uniambie haraka maana natakiwa kuondoka.”

“Hapana,” Mwanjaa akajibu.

“Asubuhi hii?”

“Pia hawajaja.”

“Sikia... naomba unichukulie begi langu pale ndani, kuna vitu vyangu vingine vidogovidogo vipo kwenye kabati.”

“Sawa kaka.”

Mwanjaa akatoka haraka na kwenda ndani. Dakika tatu baadaye, alitoka ndani akiwa na begi la Chris. Ghafla Mwanjaa akaonekana kusimama na kuonyesha kuwa na mshangao mkubwa sana.

Chris alipoangalia barabarani, akashtuka sana baada ya kuwaona maaskari wanne wenye silaha wakivuka mfereji mdogo uliokuwa pembeni mwa barabara kuu ya Dodoma – Mwanza. Pembeni waliegesha karandinga lao. Kufumba na kufumbua, taksi ilikuwa imezungukwa na maaskari wale.

“Nimekwisha!” Chris akajisemea moyoni.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Hamtakiwi kufanya chochote kwa sasa,” mmoja wa maaskari wale akasema.

“Tumefanya nini?” Chris akauliza.

“Haya mikono juu,” akasema yule askari.

Wakafanya hivyo.

Maaskari wawili kati yao, waliingia garini na kuanza upekuzi, baadaye wakamuamuru dereva afungue buti. Wakakagua lakini pia hawakuona walichokuwa wakikitafuta ambacho pia hawakusema ni nini.

“We’ dada, hiyo mizigo ni ya nani?” mmoja wao akauliza.

“Wa huyo hapo...” Mwanjaa akajibu haraka akimsonza kidole Chris.

“Lete.”

Mizigo ikapelekwa.

Haraka ikaanza kukaguliwa, Chris alikuwa akipewa maelekezo na kuambiwa atoe nguo moja baada ya nyingine na vitu vingine vilivyokuwa ndani ya begi lake.

“Wewe unaitwa nani?”

“Naitwa Dk. Christopher.”

“Unatokea wapi?”

“Dar es Salaam.”

“Unaelekea wapi?”

“Nakwenda Kiomboi,” akadanganya Chris.

“Tunaweza kuona kitambulisho chako?”

“Bila shaka.”

Mara moja Chris akatoa na kuwapa. Wasiwasi ulikuwa moyoni lakini kwa namna fulani ulianza kuondoka akiwa na imani kuwa walichokuwa wakikifuatilia kwake hakikuwa kuhusu Laura tena.

Wakakagua kitambulisho chake kisha wakamrudishia.

“Wewe dada ni nani?” askari mmoja akamwuliza Mwanjaa.

“Mhudumu.”

“Nahitaji kuona kitabu chako cha wageni,” akasema yule askari akiongozana na Mwanjaa ndani.

Alipofika getini yule askari ambaye alionekana ndiye kiongozi wao, aligeuka na kusema: “Ninyi mnaweza kwenda.”

Chris akaingia kwenye gari, dereva akawasha moto, akaondoa gari.

***

Maswali yalikuwa mengi kuliko majibu, lakini jambo kubwa kwa Chris wakati ule ni kwamba alikuwa amefanikiwa kuondoka mikononi mwa hatari ya kuingizwa kwenye kashfa ya kutembea na mke wa mtu. Yaliyoendelea nyuma hayakuwa na maana kwake.

Ndani ya Basi la Beffe, Chris alikuwa kimya kabisa, akitafakari mtihani wake uleule; kwenda kuoa kijijini.

INAENDELEA

Powered by Blogger.