KARIBU USOME HADITHI NZURI ZA KUSISIMUA

Simulizi : Singidani Sehemu Ya Tano (5)

Simulizi ya singidani
Laura alikuwa akitengeneza nywele zake saluni iliyokuwa Ginnery. Hisia zake za ndani bado ziliendelea kumhakikishia kuwa Chris ndiye angekuwa mwanaume wa maisha yake. Hakutaka kusikia mwanaume mwingine zaidi yake.

Alijiuliza, kwanini hakupokea simu yake? Kwanini hakuonekana klabu kama walivyokubaliana? Kwanini hapatikani hewani?

“Kwanini naingia kwenye mateso makubwa kiasi hiki? Nampenda Chris, nina hakika na hisia zangu. Sikutegemea kama hili lingetokea kirahisi hivi, lakini inanipasa nikubali kuwa nimeshatekwa na ninampenda. Nitahakikisha nampata Chris, lazima,” aliwaza Laura.

SAA 10:00 alasiri, Basi la Beffe lilifunga breki katika kituo cha Mkalama - Shuleni. Dk. Chris alishuka na mizigo yake. Akakodisha baiskeli iliyomfikisha nyumbani kwao.

Alipokelewa kwa shangwe na bibi yake aliyekuwa akisuka jamvi kwa kutumia  ukindu kiambazani mwa nyumba yao mpya. Walikuwa na eneo kubwa lililozungushwa kwa uzio wa michongoma. Maboma mawili makubwa ya mifugo yalikuwa pembeni mwa nyumba zao.

Walifuga ng’ombe, mbuzi na kondoo. Nyumba yao mpya iliyojengwa kwa matofali ya kuchoma na kuezekwa kwa bati haikuwafanya wabomoe nyumba yao ya asili ambayo ilijengwa kwa fito na udongo na kuezekwa kwa tembe.

“Aaaah! Mume wangu huyoo...” bibi alitamka kwa sauti kuu, akijaribu kumkimbilia mjukuu wake.

Alikuwa ajuza hasa, akiwa na umri wa miaka themanini na tatu, alimudu kufanya shughuli zake ndogondogo za kila siku. Aliishi na wanaye wawili; Shamakala ambaye alikuwa na mke na watoto wawili na Maria aliyekuwa na mtoto mmoja.

Ilikuwa famili yenye upendo mkubwa. Dk. Chris aliongeza mwendo na walipokutana na bibi yake alimpokea na kumlaza kifuani mwake.

“Ooh! Daktari wangu huyo... karibu sana baba,” bibi alisema, akishindwa kuficha furaha yake.

“Ahsante bibi, shikamoo.”

“Marhaba mume wangu, habari za nyumbani?”

“Nzuri kabisa.”

Pamoja na kuzaliwa na kukulia kijijini Mkalama, bibi huyo alimudu vizuri sana kuzungumza Kiswahili japo kuna wakati huchanganya na lugha yao ya Kinyiramba.

Mara moja bibi aliingia ndani, akatoka na kipeyu kilichojaa togwa kisha akamkabidhi Dk. Chris apooze koo na kinywaji hicho cha asili. Salamu zikaendelea.

***

Sura ya mwanamke mrembo ilimchanganya Dk. Chris, alimwangalia umbo lake. Akatazama hipsi zilizochomoza vyema pembeni ya mapaja yake, akazidi kutibuka! Matiti madogo yaliyosimama yenyewe kifuani kama embe bolibo, ilikuwa kishawishi kingine kwa Chris.

Nyongo ya huba ikapasuka. Alikiri kweli mwanamke yule alikuwa mrembo. Chris aliumia moyoni alipogundua kuwa, hawezi kumpata mwanamke yule tena. Ni Laura alikuwa akimjia mawazoni kwa kasi sana.

Akiwa amekaa chini ya mti, Chris alidongosha machozi kwa kumbukumbu za mwanamke huyo. Alitamani sana kubadilisha ukweli, awe hajaolewa lakini haikuwezekana.

“Vipi wewe?” Shamakala, baba yake mdogo alitamka akimgusa begani.

Chris alishtuka na kugeuza shingo  kumwangalia aliyemgusa. Hapo akakutana na sura ya baba yake mdogo. Shamakala akashangazwa na machozi ya Chris.

“Vipi, mbona unalia?” Shakamala akamwuliza.

Shamakala na Chris walipishana kidogo sana kiumri. Alikuwa kitindamimba katika uzao wa babu na bibi yake. Sababu hiyo iliwafanya wawe marafiki na kuelezana siri zao zote. Chris hakuona sababu ya kumficha. Alimweleza kila kitu kuhusu kisa cha Laura.

“Tulia Chris, imekuwa vizuri umegundua mapema.”

“Lakini kuna tatizo lingine kubwa zaidi.”

“Lipi?”

“Mke. Baba amesema natakiwa kurudi Dar na jibu linaloeleweka. Ameniagiza nije huku kutafuta mke, amesisitiza kwamba lazima nioe huku kwa sababu mke bora anapatikana huku kijijini.”

“Uamuzi wako ni nini juu ya hili?” akauliza Shamakala.

“Sitaki kuongozwa katika suala hili. Natakiwa kutafuta na kuamua mwenyewe nimuoe nani na wapi. Hata hivyo nilipokutana na huyo Laura, nikaona ndiye mke wangu, imekuwa tofauti.

“Si neno sana, maana siwezi kubadili ukweli ila baba sitaki kuoa huku kwa sasa, lazima nitulie kwa muda, nirudi mjini nitafute mwanamke mwingine,” akasema Chris.

“Wazo zuri, lakini mzee atakuelewa? Maana Joseph namjua vizuri sana misimamo yake.”

“Hapo ndipo ninapohitaji msaada wako baba mdogo. Itabidi tufanye mchezo. Mimi nitamwambia baba nimeshapata mke, wewe ndiye uliyenitafutia. Muda huo nitautumia kuanza kutafuta mwanamke mwingine. Unaonaje?”

“Sawa kabisa, nipo upande wako. Kaka naye pamoja na kusoma kote huko bado ana mawazo ya kizamani sana. Nitakusaidia, nipo kwa ajili yako!”

“Ahsante sana baba mdogo.”

Kilichompeleka kijijini ni kama alikuwa ameshakamilisha. Kilichokuwa mbele yake kwa wakati huo ilikuwa ni kupanga safari ya kurudi Dar. Alitakiwa kurudi haraka kwa sababu  alikuwa ameshasaini mikataba  miwili ya filamu na alitakiwa  kurekodi.

“Inabidi nirudi Dar keshokutwa.”

“Mara hii? Mbona imekuwa haraka sana?”

“Nina vimeo vingi baba mdogo, lakini usijali nitakuacha vizuri.”

“Songela sana!” (Ahsante sana) alisema Shamakala.

“Iiiza!” (Ahsante kushukuru)

***

“Jambo moja muhimu ninalohitaji kujua kutoka kwako ni kama umefanikiwa nilichokuagiza kijijini au lah!” mzee Joseph Shila alimwambia mwanaye Chris, alipomkuta nyumbani usiku huo baada ya kurudi kutoka kazini.

“Nimefanikiwa baba,” akajibu Chris, akitengeneza tabasamu la uongo usoni mwake.

“Vizuri sana. Moyo wangu sasa una amani. Bila shaka sasa tunatakiwa kufikiria kuhusu mipango ya ndoa tu!” mzee Shila akauliza tena.

Chris hakujibu!



ALIKANYAGA mafuta kisawasawa, foleni ni kama ilikuwa hakuna kabisa usiku huo. Dakika kumi tu zilitosha kabisa kumfikisha Mzalendo Pub. Akaegesha gari lake kisha akapanda hadi ghorofa ya kwanza ilipo Pub hiyo.



Hakupata shida kujua Ramsey alipokuwa amekaa maana walikuwa na kawaida ya kukaa sehemu moja ndani ya Pub hiyo kila walipokwenda. Alimfuata akiwa ameachia tabasamu mwanana.

“Vipi kaka?” Ramsey akamsalimia.

“Poa, mambo?”



“Fresh kabisa... vipi za kijijini?”

“Daaah! Huko acha tu. Yaani habari ndefu sana kaka. Nimekutana na mengi sana huko.”

“Usiniambie umepata mwanamke wa ukweli tayari... ni Mnyiramba au Mnyaturu?” akauliza Ramsey.

“Mh! Wapi ndugu yangu? Majanga tu mzee.”

“Imekuwaje?”

“Ngoja nikusimulie.”

Chris akakaa sawasawa... ni muda huo mhudumu alifika mezani kwake na kutaka kumsikiliza. Aliagiza pombe kali. Wakati mhudumu anakwenda kaunta kumchukulia kinywaji chake, Chris alianza kumsimulia Ramsey.



Hakuna alichomficha, alimweleza yote yaliyotokea Singida Mjini. Mipango waliyopanga na baba yake mdogo, Shamakala na namna alivyozugumza na baba yake baada ya kuingia Dar usiku huo.

“Aisee una kazi kaka. Yote hayo nimekusikia lakini sasa nahisi mzee mzima unaweza kuingia kwenye skendo!”

“Skendo?” Chris akahamaki.

“Ndiyo! Kama huyo mwanamke wa Singida kweli ni mke wa mtu, tena wa polisi, kuna nini tena kaka? Utachafuka!” Ramsey akasema kwa msisitizo.

Chris akabaki kimya.

Maneno yale yalimwingia akilini. Alitulia akifikiria kwa kina, akajikuta akipoteza furaha. Ni kweli alikuwa maarufu kiasi kwamba, mtu yeyote akitaka kumpata muda wowote ingekuwa rahisi tu.

“Lakini kaka, ukweli ni kwamba sikutembea naye!” Chris akamwambia Ramsey.

“Sawa ila si ulikuwa naye chumbani?”

“Kaka kuna mambo ya kisheria hapo. Hata kama nilikuwa naye chumbani, hakuna mtu aliyenikuta nikiwa naye huko chumbani. Kama ningekuwa nimefumaniwa ingekuwa sawa, lakini maneno tu ya mtaani yanaweza kunikamatisha na kuniweka ndani?”

“Kaka tunywe tu bwana!” akasema Chris kwa sauti ya kilevi.



“Ndicho kilichobaki mkubwa. Aisee nina majukumu mengi sana wiki hii. Sijui itakuwaje lakini nitajipanga,” akasema Chris.

Pombe zikaendelea. Haikuwa rahisi kwa Chris kukaa pale muda mrefu hasa kwa sababu ndiyo kwanza alikuwa ameingia Dar. Bado mawazo juu ya Laura yaliendelea kumzonga.

Alitamani sana Laura asingekuwa mke wa mtu!



***

Laura alipoteza amani ya moyo kabisa... mwanaume aliyempenda ghafla haonekani tena mbele yake. Alifikiria sana namna ya kumpata lakini alikosa majibu.

Alijiuliza maswali mengi sana, lakini mwisho alipata wazo zuri. Lilikuwa jambo gumu sana kwake lakini alikuwa tayari mradi ampate Chris.



“Lazima niende Dar es Salaam...” akawaza Laura.

Lilikuwa wazo zuri lakini lingetumia muda mwingi sana kukamilika. Alikuwa tayari kupoteza masomo japo kwa wiki moja ili aweze kumpata Chris, mwanaume wa maisha yake.

Mara moja akaanza kupanga mipango ya safari ya kwenda Dar es Salaam.



***

Laura alikuwa amedhamiria hasa. Wiki moja baadaye alikuwa jijini Dar es Salaam. Saa 11:00 jioni alikuwa anashuka ndani ya Basi la ABC katika kituo kikuu cha mabasi ya mikoani na nchi jirani, Ubungo jijini Dar es Salaam.



Alikuwa amechoka sana. Hakuwa mgeni wa Dar es Salaam. Alikuwa na ndugu zake wawili waliokuwa wakiishi jijini humo ambao kuna wakati huwa anakwenda kuwatembelea.

Mama yake mdogo aishiye Kurasini na mjomba wake anayeishi Gongo la Mboto ndiyo ndugu zake jijini Dar. Hakutaka kabisa wajue uwepo wake jijini Dar kwa sababu alikwenda kwa sababu maalum.

Alichukua taksi na kumwambia dereva ampeleke Manzese. Huko aliamini angepata gesti ya bei nafuu ambayo angeishi hapo kwa wiki nzima wakati akimtafuta Dk. Chris.

Wakiwa wanakaribia mataa ya Shekilango, Laura akavunja ukimya, alijua kwa kumtumia dereva yule angepata mwanga wa wapi pa kuanzia ili aweze kumpata Chris.

“Kaka hivi nawezaje kumpata Dk. Chris, yule mcheza filamu?” Laura aliuliza kwa sauti laini, akiyalegeza macho yake na kumfanya dereva apoteze umakini barabarani.

“Vipi unataka kumwa mwigizaji au umeshampenda bibie?” dereva yule akajibu huku akiachia tabasamu, macho yake akiwa ameyatuliza kwa Laura.

Aliporudisha macho yake barabarani, alishangazwa sana na kitu kilichotokea!

“Nakufaaa....” Laura akapiga kelele

UZURI wa Laura ulikuwa tishio, dereva alishachanganywa na uzuri wa Laura. Pamoja na urembo wa sura yake, hakuweza kuficha ushamba wake wa jiji kubwa la Dar es Salaam. Ingawa alikuwa na ndugu zake, lakini hakuwa akienda Dar mara kwa mara.

Macho ya kuangaza kila mahali, hakuweza kuyaepuka! Ni sababu hiyo ndiyo ilimfanya dereva achanganyikiwe na kutokuwa makini barabarani. Gari lilikuwa mbele yake kwenye mataa ya Shekilango hakuliona. Aliliona likiwa mita chache sana mbele yake.

Alifunga breki kwa nguvu... Laura akafumba macho ili asishuhudie ile ajali. Kwa bahati nzuri, akiwa anakaribia kabisa kuligonga lile gari, tayari magari yalishaanza kutembea... taa ya kijani ilishawaka! Hiyo ndiyo ikawa salama yao!

Taratibu wakateleza. Laura alifumbua macho, akahema kwa kasi sana.

“Weweee jamaniiii!” akasema kwa sauti dhaifu, akijaribu kuvuta pumzi ndefu sana...

Akazishusha taratibu kabisa!

“Kumbe wewe mwoga sana?” dereva yule akasema, safari hii akiwa makini sana barabarani.

“Kwani we huogopi?”

“Naogopa pia... lakini usijali. Tatizo ni wewe bwana!”

“Tatizo mimi, kivipi?”

“Tuachane na hayo, kuhusu hawa jamaa wa Bongo Movies, ukitaka kuwapata kwa urahisi ni Jumamosi mara nyingi wanakutana Leaders Club.”

“Kinondoni?”

“Ndiyo.”

“Huwa wanafanya nini hapo?”

“Si unajua tena mambo ya wasanii, wanakutana na kujadiliana mambo yao tu. Kiukweli sijui mambo yao vizuri zaidi ya hapo.”

“Ahsante, najua nitaweza kuanzia hapo. Ingia hapo kushoto, nataka kushukia hapo Tip Top.”

“Barabarani kabisa au unataka nikuingize ndani?”

“Hapana, hapo barabarani tu panatosha kabisa.”

Dereva akapinda kushoto na kuegesha nyuma kidogo ya kituo cha daladala, Tip Top. Laura akamlipa yule dereva na kubaki hapo amesimama kwa muda. Dereva akaondoa gari.

Laura aliangaza macho huku na huko, kisha akaamua kuifuata barabara ya vumbi iliyokuwa ikielekea Manzese – Uzuri. Alitembea taratibu kwa mtindo wa kuangaza huko na huko. Mbele kidogo akaona bango dogo juu ya nyumba limeandikwa Waridi Lodge.

Laura akatabasamu. Akaenda mpaka hapo, akapita moja kwa moja Mapokezi. Akapokelewa na dada mrembo sana, lakini alijihakikishia kuwa, pamoja na urembo wa dada huyo, bado hakufua dafu mbele yake! Yeye alikuwa mzuri kuliko huyo msichana!

“Nahitaji chumba,” akasema Laura.

“Umepata mrembo!”

Laura akaandikisha kwenye kitabu cha wageni. Kisha akepelekwa kwenye chumba chake.

INAENDELEA
Powered by Blogger.