KARIBU USOME HADITHI NZURI ZA KUSISIMUA

Chombezo: Mwajuma Utamu Sehemu Ya Saba (07)

"Binti utajiingiza katika matatizo huyo unayeishi naye ni mume wa mtu," aliniambia Mama mmoja niliyemfahamu kwa jina la Mama Musa.
"Si kweli," nilimwambia huku nikiamini hakukuwa na ukweli wowote.
"Shauri yako binti unachokitafuta utakipata tu," aliniambia huku akionekana kunihurumia.

Bado sikutaka kuyaamini maneno yao, niliendelea kuwa katika mahusiano na Oscar. Miezi iliendelea kukatika hatimaye mwaka huo ukapita, ulipoingia mwaka 2011 mwezi wa kwanza ndipo nilipofanikiwa kubeba ujauzito wa Oscar.
Nilifurahi sana baada ya kuubeba ujauzito huo, niliamini huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kuyaanza maisha mapya ya familia lakini ilikuwa ni tofauti kabisa na mawazo yangu.

Oscar alibadilika ghafla! baada ya kumpa taarifa hizo za ujazito, hakuwa Oscar yule niliyekuwa nikimfahamu, hakutaka kuamini kama nilikuwa nimebeba ujauzito wake, hilo lilizidi kumchanganya sana.

Nilishindwa kuelewa ni nini kilichokuwa kikiendelea, nilishangazwa na mabadiliko yake na hata nilipomuuliza nilishangaa akinigombeza na kunitolea maneno makali.
Nilihisi kuchanganyikiwa, sikutaka kuamini kama Oscar aliukataa ujauzito wake, hilo lilizidi kuniumiza sana, nilishindwa kuvumilia machozi yakaanza kunidondoka mfululizo.

Wakati nilipokuwa katika maumivu ya kukataliwa ujauzito ndipo hapohapo ambapo nilipokea maumivu mengine nisiyoyatarajia katika moyo wangu, Oscar aliamua kunieleza ukweli wa maisha yake.
Aliniambia alikuwa ni mume wa mtu na kipindi hicho mke wake ndiyo alikuwa akikaribia kurudi kutoka safarini.
Nilihisi kuchanganyikiwa baada ya kusikia maneno hayo, niliyakumbuka yale maneno niliyowahi kuambiwa na baadhi ya majirani lakini kutokana na kiburi changu sikutaka kuwasikiliza.

Mapenzi hatimaye yakaniingiza katika dunia ya maumivu na machozi, sikujua nilitakiwa kulia na nani kwani kama kuonywa nilionywa sana lakini sikutaka kusikia la mwadhini wala la mnadi swala.
“Kwahiyo unaamuaje?” nilimuuliza.
“Kuhusu nini?” aliniuliza.
“Huu ujauzito wako?”
“Mwajuma wewe ni chizi, mpumbavu, mshenzi, fala, hujielewi kabisa hivi unahisi ninaweza kuwa baba wa huo ujauzito wako? nenda katafute Baba halali lakini siyo mimi,” aliniambia Oscar maneno yaliyonifanya nitokwe na machozi. Nilishindwa kuzungumza, niliendelea kulia.

Kama ni makosa tayari nilikuwa nimeshayafanya. Kitendo cha kuishi na mwanaume bila ndoa, nikamuamini pasipokutegemea kama mwisho wa siku ningeweza kuvuna maumivu, hakika lilikuwa ni kosa kubwa mno nililolifanya.
Hatimaye Oscar aliweza kunifukuza, nikaanza kuishi maisha ya kutangatanga mitaani. Sikuwa na ndugu wala rafiki kusema labda ningeenda kumuomba hifadhi kwa muda, nilikuwa ni mimi na ujauzito wangu pekee.

Maisha yangu yalikuwa ni ya kutangatanga mitaani huku nikiomba msaada wa pesa na wakati mwingine nilikuwa nikienda kwa Mama Ntilie kuomba chakula, usiku ulipoingia nilikuwa nikilala nje, kiufupi hayo ndiyo yalikuwa maisha yangu tangu nilipoweza kufukuzwa na Oscar.


Mwanzoni niliona ugumu kuishi maisha hayo lakini kadri siku zilivyokuwa zikizidi kusonga mbele, nilijikuta nikizoea na kuona ni maisha ambayo ni ya kawaida kuishi.

Siku moja nilikutana na msichana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Savela, aliponiona alihitaji kunisaidia. Nilipojitambulisha Savela alianza kunisifia, nikashangazwa na sifa zake yaani iliwezekana vipi msichana mwenzangu kama yeye akaanza kunisifia kama mwanaume?
Hilo lilinifanya nianze kuogopa, nilihisi Savela hakuwa mtu mwema kwangu, nilipokuwa nikimuangalia nikatamani anipe pesa kisha niondoke zangu.
Baada ya Savela kunihoji na kugundua mengi yaliyokuwa yamenitokea, alihitaji kunisaidia.

Nilisita kuchukua maamuzi ya haraka lakini baada ya kujifikiria maisha ambayo tayari nilikuwa nikiishi nilijikuta nikikubali tena bila kipingamizi chochote.
Alinichukua na kunipeleka mpaka nyumbani kwake alipokuwa akiishi maeneo ya Tegeta. Kwa muonekano wa nyumba yake jinsi ilivyokuwa ikionekana ilikuwa ni vigumu kuamini kwamba Savela ndiye ambaye alikuwa mmiliki wa nyumba hiyo, hakufanania kabisa.
"Hapa ni kwako?" nilijikuta nikiropoka na kumuuliza.
"Ndiyo hii ni nyumba yangu," alinijibu huku akionekana kuwa kawaida, hakujali lolote.

"Hongera ni nyumba nzuri sana," nilimwambia huku macho yangu yakiendelea kutazama sehemu za nyumba hiyo.
"Unaishi na nani?" nilimuuliza.
"Peke yangu," alinijibu.

Ilionekana kuwa ni nyumba kubwa iliyokuwa na vyumba vingi sana, kitendo cha Savela kuniambia kuwa aliishi peke yake kilinishangaza sana, sikutaka kuamini lakini huo ndiyo iliyokuwa ukweli.
Siku hiyo ikapita huku nikiwa nimeshapata bahati ya kufadhiliwa na Savela ambaye alionekana kuwa na moyo wa kipekee sana.

Hapa ngoja nikwambie kitu, nilikuwa mchafu sana, sikuwa na nguo zaidi ya niliyokuwa nimeivaa. Siku iliyofuata Savela aliamua kunipeleka kwenye duka la nguo maeneo ya Kinondoni, tulipofika huko alininunilia nguo, alinipeleka saluni ambapo huko nikazidi kupendezeshwa, ndani ya masaa kadhaa nilikuwa nimebadilika, sikuwa Mwajuma yule mchafu ambaye nilishindia nguo moja.
"Kwanini unayafanya yote haya?" nilimuuliza.

"Usijali Mwajuma nafanya haya kama masaada wangu kwako, najua umepitia magumu mangapi, sitaki kuona ukirudi kule wakati wewe bado ni msichana mrembo, unavutia, wasichana wenzako kama wewe mjini hawafi njaa, wanafanikiwa kiulaini," aliniambia maneno ambayo aliniacha nayo njia panda.
"Unamaanisha nini?"

"Usijali muda ukifika utajua namaanisha nini au wewe hupendi kuona ukiwa na maisha mazuri, ukamiliki nyumba ya kifahari, ukamiliki gari la gharama, ukawa mfanyabiashara mkubwa sana hapa mjini yaani kila mtu akawa anakuzungumzia wewe tu?"
"Napenda ila..."
"Basi kila kitu kinawezekana, mimi binafsi nimewahi kuishi kama yako, niliteseka mno, hakukuwa na mtu wa kunisaidia yaani kama sio mimi mwenyewe kujitambua sijui leo hii ningekuwa wapi?" alisema Savela kisha akaendelea kuzunguza.

"Umeiona ile nyumba yangu ya Tegeta nimeinunua juzi tu, nafanya biashara inayoniingizia pesa nyingi mno, sijasoma lakini nimeweza kufanya vitu vikubwa ambavyo wasomi wameshindwa kuvifanya," aliniambia Savela.
Powered by Blogger.