KARIBU USOME HADITHI NZURI ZA KUSISIMUA

SIMULIZI: Sitasahau sehemu ya pili 02.

Pin by Larry Plummer on Eyes | Tears in eyes, Tears photography ...

IMEANDIKWA NA : NIHZRATH NTANI
Nikawakumbuka marafiki ambao tulikuwa tukiambizana vyumbani wakati huo tukiwa hosteli kwa furaha na kupeana matarajio makubwa ya kuwa tukimaliza chuo, tutapata kazi nzuri, tutaishi maisha mazuri na hata kuwa na familia nzuri. Kila kitu kilikuwa kinakuja kama tamthiliya fulani ndani ya mawazo yangu, nikajikuta nachukia mfumo wa ajira ya nchi yangu hata mfumo wa elimu pia, elimu inayomfanya mhitimu afikirie kuajiriwa kuliko kujiajri. Walimu wetu chuoni hawatuambii ukweli hali halisi ilivyo baada ya kuhitimu elimu yetu. Nikajikuta najichukia mwenyewe badala ya walimu hao.

Nikaanza kuwakumbuka wazazi wangu waliokuwa kijijini mkoani Mbeya, wamejenga matarajio mema juu yangu,lakini ni mwaka wa pili sasa nahangaika kutafuta kazi bila mafanikio, kila mahali nilipotuma maombi yangu hakuna nilipoitwa kwa usaili. Maisha ya kuishi kwa watu yalielekea kunichosha, hata hivyo si mimi tu hata walezi wangu walianza kunichoka. Nikaanza kuchukia ni kwanini nilitumia muda wangu mwingi kusoma, kusoma kusiko na faida?

Kutokuwapo na kazi yenye kuniingizia kipato kukapelekea nimpoteze 'My Girlfriend' Binti yule wa Kimanyema niliyekuwa nafikiri ananipenda kwa dhati, kumbe alikuwa ananidanganya. Mwanamke niliyempata Chuoni, nilimpenda kweli kweli lakini baadae aliniacha kwa sababu sina pesa. Wako wapi wanaosema pesa haina umuhimu katika mapenzi?.Mnajidanganya.


Nikaanza kuyakumbuka matendo yake kwangu, nyakati fulani alilia kwa ajili yangu hasa nilipomuuzi, alinihakikishia kuwa mimi ni wake na yeye ni wangu mpaka ndoa na hakuna kitakachotutenganisha. Kumbe nilikuwa napumbazwa ndani ya dimbwi la mahaba. Mahaba yaliyokuja kuniumiza baadae. Nikajikuta nikiwachukia viumbe hawa wanaoitwa wanawake. Hata hivyo, bado moyo wangu haukuepa maumivu yale.

Sauti ya konda ilinigutusha kutoka katika lindi la mawazo yale, tayari gari limewasili kituoni, kituo kilicho pembeni na uwanja wa ndege. Haraka nilishuka nikaanza kutembea. Sijui ni kitu gani kilinifanya nigeuke nyuma kabla ya kuvuka barabara. Nikajikuta nabakia na mshangao mkubwa! .

Ndio! macho yangu yakakutana na binti yule mwokozi wangu, binti aliyenionea huruma na kunilipia nauli ndani ya Bus . Haraka nilimpa tena asante kwa msaada wake, binti yule akanijibu "nisijali", nilimuuliza wapi anapoelekea, alinijibu yeye ni mgeni mahali hapo na amekuja kumsubiri mgeni wake kutoka nje ya nchi, hata hivyo amewahi sana, atafika hapo masaa mawili baadae.

Binti yule aliniomba nimuoneshe mahali panapopatikana chips nzuri apate kula, ni baada ya kumwambia mimi ni mwenyeji mahali hapo. Nikachukua jukumu la kumsindikiza, nilimpeleka kwenye Cafe zilizoko pale karibu na kituo cha tax. Baada ya kufika pale nilianza kumuaga kwa minajili ya kuondoka. Binti wa ajabu alipinga uamuzi wangu, akaniomba tuwe pale tupate wote chakula na kinywaji kisha angeniruhusu kuondoka kama sitajali. Kumbuka sikuwa nimetia chochote tumboni kwa wakati huo, hakika sikujivunga.....nikavuta kiti na kukaa.

Kuwepo kwangu na binti yule mahali pale kukapelekea kutambuana, alinifahamisha kuwa anaitwa Nadia, ni sekretari wa kampuni moja ya Bima nchini na yupo pale kwa ajili ya kumpokea rafiki yake mmoja. Nilijitambulisha kwake kuwa naitwa Richard Kamba. 

Nilimuelezea maisha yangu kwa ufupi, hata hivyo sikuwa natambua kwanini namuelezea maisha yangu mtu nisiyemfahamu? Hata hivyo nguvu fulani iliniambia nimefanya jambo sahihi kwa wakati ule.

Baada ya muda tuliachana na binti yule, alinipa 'Bussines Card yake', akinisisitiza kuwa nikifika nyumbani nimpigie, maana simu yangu nayo ilikuwa imeibiwa kwa tukio lile la Posta. Vile vile alinipatia noti ya elfu tano, bahati ilioje? kwa dakika zile nikajikuta nasahau yote uso ukajaa tabasamu. Nilipofika nyumbani nilioga na kupata chakula nilichokikuta, kazi ya kutazama vipindi vya television ikachukua nafasi yake kama ilivyo siku zote. Hiyo ndio ilikuwa kazi kubwa nikiwa nyumbani, kushinda kwenye tv.

Baadae nilipokumbuka kumpigia simu Nadia, nikatafuta 'Bussines Card' ile bila mafanikio, sikumbuki wapi nilipoiweka, nilitafuta mwishowe nilikata tamaa. Na sikuiona tena.

Maisha ya hapo nyumbani hayakuwa yenye furaha kwa upande wangu hata kidogo, sikuwa na kazi ya kufanya na muda mwingi niliutumia kukaa sebuleni na kutazama tamthiliya za kifilipino na baadhi ya filamu za Bongo movie yalikuwa maisha yangu ya siku zote. Maisha ya mtu hasiye na kazi.


Mwaka sasa, bado ningali natafuta kazi na hakuna mahali nilipowahi kuitwa hata kwenye usaili tu. Walezi wangu walianza kunichoka taratibu hapo nyumbani nilianza kufikiria kurudi kijijini, mahali walipo wazazi wangu, hata hivyo bado moyo wangu haukuwa radhi kurudi Tukuyu. Sikuweza kukata tamaa. Tukio la ajabu likatokea....

***********************

ITAENDELEA

Powered by Blogger.