KARIBU USOME HADITHI NZURI ZA KUSISIMUA

Simullizi: Sitasahau sehemu ya kwannza (01)

Pin by Larry Plummer on Eyes | Tears in eyes, Tears photography ...
IMEANDIKWA NA : NIHZRATH NTANI
Nikiwa ndio kwanza nimetoka kutuma barua ya maombi yangu ya kazi, kwenda kwenye kampuni moja inayohusika na usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi. Asubuhi hii ilinikuta niko maeneo ya Posta, jijini Dar es salaam. Kuwepo kwa mvua za rasha rasha zilinifanya nijumuike na watu wengi kujificha pembezoni mwa korido za ofisi zilizoko maeneo hayo. Hata hivyo, baada ya muda fulani mvua zile zilikata.

Nikaanza kujivuta kusogea stendi ili nipate usafiri wa kurudi nyumbani ninapoishi pale maeneo ya Ukonga Airport. Kwa muda ule wa asubuhi ya saa nne hakukuwa na shida yoyote ya usafiri kama ilivyo adha la jiji la Dar Es Salaam, magari yalikuwa mengi. Wakati nalifuata basi moja kati ya mabasi machache yaliyokuwepo kituoni hapo yanayokwenda njia ya Gongolamboto. Nikajikuta namgonga kwa bahati mbaya mdada nisiyemfahamu.Mungu wangu!


Bila kutarajia, macho yangu yakajikuta yakiangalia baadhi ya nyaraka zilizosambaa ardhini kutokana na kitendo kile nilichokifanya bila kukusudia, nikajikuta mwili wangu ukiinama na kuziendea nyaraka zile na kuzikusanya kwa uangalifu mkubwa. Sikuwa najua nini kilichoifadhiwa ndani ya nyaraka zile. Kwa unyonge niliyainua macho yangu na kumtazama binti yule kwa mara ya kwanza, nakiri kabla ya hapo sikuwa nimemtazama vizuri binti huyu.

Macho yangu yakatua kwenye uso wa binti yule, Lalaula! nikashtuka! ni kama nimeshikwa na bumbuwazi kwa muda wa sekunde chache, mapigo ya moyo wangu yalikimbia kwa maili nyingi. Kitendo kile kilifanyika kwa haraka mno. Hata hivyo niliweza kumkabidhi binti yule nyaraka zile, na alipozipokea tu alinisindikiza na tusi na msonyo juu yake, nikabakia kufadhaika kwenye macho ya watu wengi, mvulana mimi!.

Wakati macho yangu yakimsindikiza binti yule akitokomea ndani kabisa ya Bank ya CRDB tawi la Azikiwe lililopo jirani na eneo hilo la Posta hapa jijini Dar es Salaam. Nami nikajivuta na kuingia ndani ya Bus, na kukiendea kiti cha kati kati upande wa dereva kisha nikakaa hapo. 

Dakika chache baadae basi lile likaanza safari. Mawazo ya binti yule yakaanza kunitawala. Hakika alikuwa binti mzuri ajabu na mrembo hasa wa kupendeza ambaye nakiri sikuwahi kukutana na msichana mzuri kama yule kabla. Kila kitu kilichotokea kwa dakika zile chache zikawa zinajirudia mawazoni mwangu. Nikajikuta najiuliza kwanini binti yule atawale mawazo yangu?.Nikakosa jibu.

*****************
Milio ya 'coins' kama ilivyo ada ya makonda wengi wanavyozichezesha pesa hizi za 'silver' kwa mtindo wa kipekee kabisa, ilinigutusha kutoka katika lindi la mawazo kwa wakati huo. Konda alikuwa ananikumbusha nimpe pesa yake, huku macho yangu yakitazama nje, nikaja gundua tupo kwenye foleni ya kuvuka mataa pale Tazara. Haraka nikaingiza mkono wangu mfukoni ili nitoe akiba yangu nimlipe konda yule.

Hamadi! mikono yangu ilirudi patupu, hakukuwa na pochi wala pesa. Nikajikuta natafuta kila mahali ndani ya mifuko ya suruali yangu kama mtu aliyechanganyikiwa kwa muda huo lakini majibu yalikuja yale yale, pochi haikuwepo. Nikajikuta nababaika huku nisijue cha kufanya. Wakati huo huo konda alikuwa yupo makini na mimi akisubiria nimpatie haki yake. 

Kwa mara nyingine tena, nikawaza! nikawaza! nikahofu kufadhaika ndani ya Bus. Kwa ujasiri wa kiume nilimjibu konda yule, nimeibiwa pochi na pesa iliyokuwemo. Konda hakunielewa hata kidogo, akaanza kutoa maneno ya kashfa na ya udhalilishaji juu yangu, huku akisema ni tabia za vijana wengi kusingizia kuibiwa mara wanapodaiwa nauli. Nikafadhaika!

Maneno yale yalinifanya niwaze sana, nikaanza kujiuliza nikiwa msomi wa shahada moja ya elimu ya teknolojia, leo nadhalilika kwa kutokuwa na shilingi mia nne tu ya nauli? Konda yule akawa anaendelea kusisitiza kuhitaji nimlipe nauli yake. Dada mmoja kama malaika akajitokeza pasipo tarajia;...wakati nikiwa nimebakia nafikiria kumwambia konda anisaidie huku nikiwa na hofu kutokana na matamshi yake dhidi yangu, nikajikuta nadhamiria kumuomba anishushe.

Hata hivyo kabla ya kuyasema hayo, nikasikia sauti ya kike kutoka nyuma ya kiti changu ikimwambia konda akate nauli yake na yangu. Haraka niliyageuza macho yangu na nikajikuta yanagongana na ya msichana mrembo wa haja. Bahati kubwa hii? Nilijiuliza. Haraka nilimjibu "Asante" nae akaachia tabasamu machoni mwake huku akinijibu "husijali kaka", Wakati huo huo konda alikuwa anarudisha chenji kwa yule dada. Safari ikaendelea.

Nikajikuta mawazo yangu yanamkumbuka yule dada niliyemgonga pale posta, nikaanza kuhisi kuwa tukio lile lilipelekea kuibiwa pochi yangu bila kufahamu, sikumbuki ni muda gani nilibiwa lakini najua kuna mvulana alikuja na kumuuliza yule dada tatizo mahali pale. Wakati naendelea kuwaza...nikaanza kuwaza maisha yangu chuoni.

INAENDELEA

Powered by Blogger.