KARIBU USOME HADITHI NZURI ZA KUSISIMUA

SIMULIZI : Sitasahau sehemu ya tatu (03)

Pin by Larry Plummer on Eyes | Tears in eyes, Tears photography ...

Miezi miwili baadae nikapokea simu ya mdada mmoja huku akihitaji kuzungumza na Richard, bila shaka niliipokea simu ile na kuzungumza nae kwa umakini mkubwa, ndipo alipojitambulisha anaitwa Aisha ni Katibu Muktasari wa kampuni ya Tanzania Transport company, akinipa taarifa ya kuitwa kwenye usaili siku ya jumamosi ofisini kwao kutokana na maombi ya nafasi ya kazi niliyoomba miezi michache iliyopita. Hakika ilikuwa tukio lenye kuleta furaha sana kwa upande wangu. Nikaazimia kushinda usaili huo.

Jumamosi kwa upande wa Dar es salaam mara nyingi nyakati za asubuhi huwa hakuna shida ya usafiri, lakini mimi saa moja kamili ilinikuta nimeshafika Msasani mahali ilipo ofisi za Kampuni ile, nakiri kabisa sikuweza kupata usingizi usiku wa kuamkia siku yangu ya usaili. Hata hivyo niliwahi sana maana ofisi ile ilikuwa inafunguliwa saa mbili na nusu asubuhi na usaili ulipangwa kufanyika saa nne asubuhi, sikujali sana umbali wa muda huo. Nikasubiri kwa hamu kubwa.

Baada ya kuvumilia sana huku nimekaa na watu nisio wafahamu malengo yao, tukaja kuitwa wale wote waliotakiwa kufanyiwa usaili siku hiyo, ndipo nikatambua sikuwa peke yangu, tulikuwa kama watu sita hivi. Nikasogea na kukaa kwenye chumba ambacho kilitengwa maalumu kwa shughuli hiyo. Tukakaa kwenye benchi ya kisasa lililopo pembeni ya chumba kwa ajili ya kusubiriwa kuitwa. Muda Ukawadia na nikapigwa na bumbuwazi.

Nilikuwa mtu wa kwanza kuingia chumba cha usaili, ikiwa ni mara yangu ya kwanza kufanyiwa usaili tangu nilipoanza kutafuta kazi, hivyo suala la hofu sikuweza kuepukana nalo. Hofu ikanitawala. Ni wakati ambako nilisikia sauti kwenye masikio yangu ikiniambia "Richard ondoa hofu uliokuwa nayo, jiamini kwa sababu hii ni nafasi muhimu ambayo umeipata, shinda hofu hii" Kauli hiyo ilisambaa kwa kasi ya ajabu masikio mwangu, haraka nikashusha pumzi kwa nguvu zote. Wakati huo tayari nipo ndani ya chumba kizuri ajabu.

Chumba chenye kunakshiwa na rangi nzuri na vitu vya thamani kubwa. Chini ya chumba kile kulitandikwa zulia zuri jekundu, pembeni ya ukuta kulikuwa na tv nzuri ya kisasa iliyokaa vyema ukutani pale. Macho yangu kwa kasi ile ile yakaendelea kusawiri chumba kile. Hakika ni chumba kilichokuwa kinavutia sana kwa harufu nzuri iliyosambaa chumbani mle ,huku hali ya kiubaridi ikitawala eneo lile. Wakati ukawadia.

Wakati nikiendelea kustaajabu uzuri wa chumba kile ghafla sauti ya kike ikasikika " Naitwa Tayana Masenga ni Afisa Uajiri wa kampuni hii na nipo hapa na Afisa habari Mr Salim Mhando, karibu sana ndugu" Wakati huo nilimuona yule dada akivua mawani yake kwa utulivu husio kifani. Ni wakati huo huo macho yangu yalipokimbia maili nyingi kwa kasi ya ajabu na kutua usoni mwa msichana yule. Nikashtuka! Sikuamini macho yangu kwa wakati ule.

Haraka kumbukumbu zangu zikarejea kwa kasi ya ajabu, nikajiuliza wapi nilimuona binti huyu? wakati huo huo mapigo ya moyo wangu yakawa yameongezeka kwa kasi isiyo ya kawaida. Ni wakati ambapo moyo wangu ukahisi hali ile ile, hali ambayo niliwahi kuhisi kipindi fulani uko nyuma. Naaam! haraka nikamkumbuka..."Ndiye huyu! ndiye yeye hasa" Nikajiambia...

.Ni binti yule yule ambaye nilikutana nae Posta na kumgonga kwa bahati mbaya tu kama nilivyohisi kwa upande wangu , ni binti huyu ambaye alinifanya nipewe maneno ya kashfa na konda. Ni binti huyu ambaye alinifanya nipoteze simu yangu ya thamani wakati wa tukio lile, kumbe anaitwa Tayana? nikajijibu.

Badala ya kuanza kumchukia nikajikuta nabakia kutabasamu..tabasamu la uongo. Tabasamu la kihisia! nikajikuta najitambulisha..."Naitwa Richard Kamba na nipo mahali hapa kwa ajili ya usaili" Wakati najitambulisha macho yangu yalikuwa yanamtazama binti yule ambaye naweza kusema kwa wakati huo ni adui yangu. Hata hivyo sikuona chochote kilichobadilika usoni kutoka kwa binti yule mrembo. alionesha sura ile ile yenye kuvutia. Ajabu ilioje?

***************
Nilianza usaili ule kwa kujibu kila swali kwa umakini mkubwa na uwerevu wa hali ya juu, majibu yangu yalionekana kumfurahisha sana Afisa habari wa kampuni ile, wakati wote kila nilivyokuwa nikijibu kwa umahiri mkubwa alikuwa akibakia akitabasamu na huku akiandika kitu nisichokifahamu kwenye 'Note Book' yake. 

Ndipo binti yule mrembo aliponiuliza swali ambalo lilionekana kama la mwisho kwa upande wangu. Aliniuliza: " Unataka ulipwe mshahara kiasi gani?" Hakika lilikuwa swali gumu kulijibu na kuna sauti nikaisikia masikioni mwangu ikinisisitiza nilijibu swali hilo kwa uangalifu wa hali ya juu.

INAENDELEA

Powered by Blogger.