KARIBU USOME HADITHI NZURI ZA KUSISIMUA

SIMULIZI: Sitasahu sehemu ya Nne (04)

Pin by Larry Plummer on Eyes | Tears in eyes, Tears photography ...

Nikajibu: " Napaswa kulipwa kutokana na kiwango ambacho kampuni hii imekitenga kwa ajili ya nafasi ninayoiomba. Napaswa kulipwa kutokana na utendaji wangu na kiwango cha faida nitakachokiletea kampuni. Pia napaswa kulipwa kutokana na kiwango cha elimu yangu" Nikamaliza kulijibu swali lile. Na kuwatazama wale watu wote wawili walio mbele yangu. Nilimuona yule afisa habari akitabasamu na kumuangalia binti yule kwa furaha hata hivyo sura ya binti yule ikabakia vile vile katu haikujibu tabasamu la afisa habari yule. Nikafadhaika!

Baada ya usaili niliruhusiwa kuondoka mahali pale huku yule afisa habari akinipa pongezi za kipekee na kunipa matumaini makubwa juu yangu ya kupewa ajira katika kampuni ile.Tofauti na yule binti mrembo yeye aliguna tu. kisha akafunga kitabu chake na kuvaa miwani yake ambayo ilionekana wazi ni ya matatizo ya macho. Nilitoka ndani mle nikiwa nusu nina furaha na nusu nikiwa na huzuni, hasa nikikumbuka kuwa binti yule mrembo alikuwa ni kama ufunguo wa ajira yangu, ni yeye ndie atakayeamua nafasi yangu. Nikasali! nikasali! nikasali kwa Mungu wangu nishinde usaili ule.

**************
Wiki zikapita, hadi miezi ikapita, sikuwahi itwa na kampuni ile kwa ajiri ya ajira. Hakika nilikata tamaa kabisa ya kuajiriwa na nikatamani kujiajiri mwenyewe hata hivyo nilikosa mtaji wa kuanzisha biashara. Mjini nikapaona pachungu huku manyanyaso yakizidi toka kwa walezi wangu. Maisha yalikuwa magumu sana kwa upande wangu. 

Mwanaume mimi nilikosa hata pesa ya vocha. Wakati mwingine nilitegemea chenji zinazotokana na mahitaji madogo madogo ninayotumwa kwenda kununua na kiasi kidogo kinachobakia ndio hutumia kununua vocha. Nilikata tamaa ya maisha. Nikazidi kuchukia muda wangu niliyoupoteza kuitafuta elimu. Wakati ukawadia.

Ni siku chache baadae nikaliona tangazo kwenye gazeti la serikali kuhusu nafasi za ajira kutoka shirika la Ethiopian Airline, ambalo limefungua tawi hapa nchini. Niliandika maombi yangu na kuambatanisha CV yangu yenye nyaraka kivuli za kuthibitisha kile nilichokiandika kwenye wasifu wangu na bila kuchelewa nikatuma. Wiki moja baadae niliitwa kwenye usaili.

Baada ya wiki moja kupita nilipokea simu ya kuhitajiwa ofisini kwa kupeleka nyaraka zangu halisi ni baada ya kuelezwa kushinda usaili niliyofanya. Kila kitu kilienda kama simulizi nzuri ya kuvutia ni kama kusoma vitabu vya Robson Kruso. Hatimaye nikaajiriwa rasmi kama Afisa wa IT yaani 'Information Technology' katika shirika hilo. Kumbuka nina shahada ya kwanza ya IT kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam. Maisha yakaanza kwa upande wangu.

Nilianza kazi kwa juhudi kubwa na kujituma kusiko kwa kawaida huku nikiazimia kufidia muda wangu nilioupoteza kwa kipindi chote. Miezi minne baadae niliomba kuhama na kuanza maisha ya kujitegemea. Ilikuwa jambo gumu kwa walezi wangu kunielewa hawakupenda kuhama kwangu kwa haraka kwa kipindi hicho. 

Nilijaribu kuwashawishi na mwishowe wakakubaliana na uamuzi wangu. Wakati huo huo nikaanza kujiuliza inakuwaje sasa wananipenda, wananililia nikae pale ilhali kipindi sina kazi walikuwa wananinyanyasa? Huku wakinishinikiza nirejee kijijini ....Nikagundua kuwa ni kwa sababu ya kazi yangu, nikasema kwa sababu ya pesa. Hakika pesa ni kila kitu "Nikawaza".
Nilipanga chumba na sebule eneo la Mbezi Kimara, mbali na mahali walipo walezi wangu. 

Sikutaka kukaa karibu nao. Nilitaka kuwa huru zaidi katika eneo jipya. Miezi michache baadae nilibahatika kupata mkopo ambao niliutumia kununua vitu vya ndani kama Tv, fenicha za kisasa na vingine vingi. Sasa chumba changu kikaanza kuwa na mwonekano mzuri na wenye kuvutia, chumba anachostahili kuishi mvulana wa kisasa. Pia ukumbuke kwa kipindi hicho sikuwa na msichana hata mmoja, hakika niliwachukia wanawake . 

Kila siku inayokwenda , nilimuomba Mungu anioneshe mke wangu kwa sababu wakati huo sikuwa nawaamini wanawake tena pamoja na kukutana na vishawishi vingi kwa wakati huo.

******************************
Mwaka mmoja baadae kupitia akiba niliyokuwa nikijiwekea nilifanikiwa kununua kiwanja maeneo ya Kigamboni. Nilianza kufurahia maisha na hata mwonekano wangu ulianza kubadilika. Nilikuwa mvulana mtanashati sana, kila mmoja aliyepata kuniona kabla ya kuajiriwa alibaki akipigwa na bumbuwazi mara tu alipopata bahati ya kukutana nami kwa wakati huu. Nilikuwa mwaminifu na mtiifu sana kazini.

INAENDELEA

Powered by Blogger.