KARIBU USOME HADITHI NZURI ZA KUSISIMUA

SIMULIZI: Sitasahu sehemu ya Nane (8)

Pin by Larry Plummer on Eyes | Tears in eyes, Tears photography ...
Hakuniambia, akanijibu si wakati wake, ila siku moja ataniambia. Hakika siku hiyo tuliongea mengi zaidi na baada ya muda tukajikuta tumekuwa marafiki. Baada ya chuki faraja nikatambua. Hata hivyo kuhusu kazi yangu sikumwambia ukweli. Aliponiuliza kuhusu ninafanya shughuli gani kwa sasa? Nilimjibu kuwa nafanya kazi shirika la ndege la Ethiopian nikiwa mfanyakazi ninayehusika na mifumo wa mawasiliano ofisini hapo. Baada ya kutumia masaa machache hapo, sote kwa pamoja tukarejea hotelini.

Urafiki wetu ukadumu na kuimarika sana, kila mahali tulikuwa pamoja. Sasa nikahisi nimepata mwenyeji, mwenyeji binti mrembo. Kwa siku tatu hata wahudumu wa hoteli hiyo walikuwa wanatutania kuwa tumependeza sana kama mtu na mke wake. Maneno hayo yalikuwa yakituingia moja kwa moja ila sote tuliishia tukitabasamu kwa furaha, Tabasamu lenye kumaanisha jambo. Mpaka hapo tulikuwa marafiki tu.

Likizo ilipokuwa inafikia tamati. Likizo ya wiki moja ambayo nilipewa na shirika baada ya kupandishwa cheo kazini na nitakaporejea nirejee katika majukumu mapya. Makubwa zaidi niliyokuwa nayafanya mwanzo. Nilimweleza kila kitu Tayana kuhusu kuisha kwa likizo yangu hivyo nitawajibika kurejea Dar es salaam kuendelea na majukumu yangu ya kikazi.

Uamuzi wangu ulionekana kuwa wa ghafla sana kwake. Nikauona uso wake ukipoteza ile nuru ya furaha niliyoizoea siku zote huku akiachia tabasamu hafifu machoni pake. Nikahisi hakutegemea uamuzi wangu kwa kipindi kile. Kipindi ambacho alianza kusahau kila kitu kuhusu matukio ya maisha yake ya nyuma yaliyopelekea apoteze sio tu furaha yake hata amani ndani ya moyo wake.

Tayana akawaza sana kisha akanijibu kuwa kwa kipindi tulichokuwa pamoja ametambua wazi mimi nina umuhimu mkubwa kwake....ni mimi ndiye niliyemsahulisha na mawazo mengi yaliyopelekea kutaka kufupisha uhai wake hivyo katu hataweza kubaki peke yake yu radhi naye kufupisha likizo yake na kuongozana nami kurejea Dar es salaam kama tu nitakuwa radhi kuongozana naye. Machozi yalionekana yakimtiririka kwenye mashavu yake, nikashtuka! Nikajikuta namuuliza kwanini analia?


Ndipo aliponieleza kuwa alipewa likizo na kampuni kwa ajili ya kupunguza mfadhaiko uliomkumba baada ya kuachana na mwanaume aliyempenda sana. Mwanaume ambaye siku zote aliamini kuwa ndiye atakayejenga nae familia siku za usoni. Mwanaume ambaye siku zote alimuamini na kumpenda. Mwanaume ambaye alimfanya ajisikie mwenye furaha kila wanapokuwa pamoja. 

lakini kila kitu kilikuja kubadilika ndani ya usiku mmoja tu. Pale mwanaume huyo ambaye alimwambia kuwa kila kitu kati yetu kifikie tamati leo. Tayana hakuwa na namna tena, alilia na kuuliza sababu lakini mwanaume huyo akamjibu hana sababu. Maumivu ya moyoni yakamtawala kwa wakati huo. Mapenzi yakamuumiza Tayana .

Siku mbili baadaye tulikuwa sote mimi na Tayana tulikuwa ndani ya Boti ya Kilimanjaro kurejea nyumbani huku nyuso zetu zikitawaliwa na tabasamu lenye kuvutia sana. mazungumzo yetu yalitawaliwa na vicheko vya hapa na pale. Ni kama tunakutana kwa mara ya kwanza huku kila mmoja akimuhitaji mwenzake, kwa upande wangu halikuwa jambo nililowazia kwa wakati huo. Nikasahau kama tupo safarini. Tena juu ya maji....Safari ikawa fupi ajabu.

Masaa mawili kasoro baadae tuliwasili salama bandarini Dar es salaam. Baada ya kumaliza hatua zote muhimu tuliagana mimi na Tayana. 

Tukikubaliana kuendelea kuwasiliana kwa kadiri iwezekanavyo. Wakati anapoelekea kupanda gari iliyokuja kumchukua eneo hilo huku macho yangu yakimsindikiza binti huyo ghafla bila kutegemea, Tayana aligeuka nyuma mita chache niliposimama na mita chache iliposimama gari ikimsubiri. Tukatazamana! Macho yetu yakagongana ...macho yakatoa ishara , ishara ya kihisia. Nikatabasamu naye akanijibu kwa tabasamu. Tabasamu lake likanifanya nicheke naye akacheka. Nikampungia mkono kama ishara ya kumuaga kwa mara nyingine tena naye akapokea ishara yangu na kuingia garini.

Nami nilielekea kwenye gari iliyokuja kunichukua na kunipeleka nyumbani kwangu. Mawasiliano yangu na Tayana yaliendelea kuimarika kila siku. Ikafikia hatua siwezi kulala bila kusikia sauti ya Tayana naye pia hivyo hivyo hawezi kulala bila kusikia sauti yangu. Tukaendelea kuwa karibu zaidi huku kila wikiendi tulikuwa tukikutana sehemu mbalimbali.Mpaka kufikia kipindi cha miezi miwili hakuwa anapajua nyumbani kwangu, kila wakati aliniletea ombi la kuhitaji kunitembelea nyumbani kwangu kila mara nilitoa visingizio vingi. 

Sikutaka apajue nyumbani kwangu kwa wakati huo. Maana nilikuwa naendelea kumalizia ujenzi wa nyumba yangu kisha nihamie hapo na ndipo ningeweza kumkaribisha kwangu. Ndivyo nilivyopanga siku zote. Mpaka kufikia hapo hakuna aliyepata ujasiri wa kumueleza mwenzake hisia zake. Sote tukaacha matendo pekee yazungumze.


Miezi mitatu baadaye tangu kumfahamu na kujenga ukaribu kati yangu na Tayana. Nilikuwa mimehamia nyumbani kwangu. Nyumba yangu haikuwa imekamilika kila kitu kama nilivyotaka ila kwa kiwango ilipofikia haikunizuia kutohamia hapo. Hapo ndipo ndoto yangu ya kwanza ya kumiliki nyumba nzuri ya kisasa ikatimia.Nikasahau matatizo yote ya nyuma. 

Wakati mwingine nilipokuwa nayakumbuka maisha yangu ya nyuma nilijisikia kuumia sana. "Katu husiyakumbuke ya nyuma maana yanaumiza sana" Nilisikia sauti ikiniambia masikioni mwangu. 

Kumbuka mpaka kufikia hapo nilishaenda zaidi ya mara moja nyumbani kwa Tayana. Hakika Tayana alikuwa msichana wa kisasa, mwenye kumiliki nyumba ya kisasa katika umri wake ilikuwa jambo gumu kuamini. Zaidi ya hapo nilipigwa na butwaa baada ya kuyaona magari matatu ya kifahari yaliyopaki ndani ya uzio wa nyumba yake. Magari ya ndoto yangu, nilijisemea. Tukio la ajabu likatokea.........

Inaendelea

Powered by Blogger.