SIMULIZI: Sitasahu sehemu ya Saba (7)
Hakika niliongea na muhudumu
na kunifanyia Booking ya chumba cha stahiki yangu. Baada ya yote hayo
nikajiuliza ni usafiri gani ambao ningeutumia kwenda huko kati ya Ndege au
Boat. Hapo nilikuwa na uamuzi wa haraka sana. Sikuwahi safiri na chombo
chochote cha majini nikaona hii ni fursa ya kipekee kutimiza ndoto hizo.
Usafiri wa Boti ukawa chaguo lisilo na upinzani.
Bila kuchelewa, asubuhi ya saa kumi na mbili
nilikuwa barabarani naelekea bandarini kwa ajili ya safari hiyo. Kutokana na
foleni kubwa ya Dar Es salaam nikajikuta nakosa usafiri wa saa moja. Hivyo
nikapata usafiri wa saa tatu na nusu asubuhi. Ni baada ya kupata tiketi kutoka
ofisi za Azam Merine zilizoko hapo hapo Bandarini.
Saa tatu na nusu tayari nimo ndani ya Boti ya
Kilimanjaro nikielekea Zanzibari. Hakika ilikuwa safari nzuri sana kwangu
ukizingatia ilikuwa mara yangu ya kwanza kutumia usafiri wa majini. Pia
sikuweza kukaa ndani kutokana na hofu ya kutapika. Basi nikakaa juu kabisa
ambako kuna hewa na upepo unapatikana kwa wingi. Upepo ambao ulinisaidia
nisitapike.
Masaa mawili baadae nilikuwa nateremka bandarini
Unguja, kila abiria alikuwa mwenye furaha kubwa ya kufika salama. Nje ya geti
nikaiona gari yenye maandishi ya Hoteli ya Melia na pembeni yake kuna mwanaume
ameshika bango lenye jina langu kuwa yeye ndiye atakayenipokea. Nikamuendea na
kujitambulisha kwake huku nikitoa kitambulisho na kumkabidhi mtu yule. Haraka
alichukua begi langu dogo na kuweka mlango wa nyuma ya gari lake kisha
akanifungulia mlango wa mbele pembeni yake. Kitabia huwa sipendi kukaa mbele
katika chombo cha moto labda mimi niwe ndie Dereva. Huwa navutiwa kukaa nyuma
zaidi kwa imani kuwa inapotokea ajali ni nadra mtu wa nyuma kupata tatizo na
hata akipata huwa bahati sana kufa. Imani niliyokuwa naishikilia kwa muda mrefu
sasa.
Siku hiyo nilipenda kukaa pembeni ya dereva. Ni
uamuzi huo uliokuja kunipa furaha kubwa maana niliweza kuyasawiri maeneo mengi
ya Zanzibar. Huku nikistaajabu na hali ya ukimya niliokuwa naushuhudia
barabarani. "Hakika Zanzibar ni mji wenye kuvutia sana" Nilijisemea.
Wakati naendelea kuangalia mandhari ya mji wa Zanzibar nilikuja kushtukia tunafunguliwa
Geti la Hoteli ya kisasa ya Melia. Kwa nje ilionekana hoteli nzuri sana kwa
jinsi ilivyopambwa kwa namna ya kipekee kabisa. Jambo hilo likanifanya niwe na
shauku ya kuingia ndani humo.
Ni baada ya dakika chache ya kufanya malipo,
ndipo nilipokabidhiwa chumba cha kisasa kabisa ambacho kilinifanya niupongeze
uamuzi wangu wa kuichagua Hoteli hii kwa ajili ya likizo yangu fupi. Nikajitoma
Chumbani. Siku hiyo sikutoka nje ya Hoteli hiyo. Muda mwingi niliutumia kusoma
na kutazama Tv. Siku zikasonga, muda ukatimia na majibu ya maswali yangu
yakapata majibu.
Baada ya siku tatu tangu niwasili hapa Zanzibar
na siku mbili nilizitumia kutembelea maeneo ya kihistoria. Nilianza kupapenda
Zanzibari. Ilikuwa ni siku ya nne nyakati za asubuhi sana kama kawaida.
Niliamka na kutoka nje ya Chumba changu kwa ajili ya kufanya mazoezi. Sikumbuki
ilikuwa muda gani ila bado nakumbuka kila kitu. Ilikuwa kati ya saa moja
asubuhi na saa mbili.
Nikiwa nimevalia mavazi ya kimazoezi baada ya
kukimbia pembezoni mwa bahari na kuchoka sana. Ndipo nilipokuwa narejea
taratibu kwa mwendo wa uchovu kutoka pwani ya Bahari mwa hoteli ya Melia.
Macho
yangu yakanasa kiumbe kilichokuwa kimejilaza kwenye kiti cha uvivu ambacho
wazee wengi wa maeneo ya Pwani hupenda sana kuvitumia viti hivyo...viti vya kulala
ambavyo mara nyingi vinakuwepo maeneo ya beach zile kubwa na za gharama.
Msisimko wa ajabu ukatawala mwili wangu ,nikajikuta nashikwa na bumbuwazi!.
Na kwa mara ya kwanza moyo wangu ukavutiwa na
kiumbe kilicholala kama mita arobaini kutoka nilipo. Sijui kwa namna gani macho
haya yaliweza kunasa kiumbe hicho. Ni wakati ambapo nikaanza kupoteza kujiamini
kwangu. Nikajikuta hisia za uwoga zikianza kutambaa mwilini mwangu kama vile
kitu fulani kibaya nimekiona. Nikajikuta moyo na macho yangu yakihitaji
kuendelea kumtazama kiumbe huyo. Huku akili haikuweza kuhama kwenda sehemu
nyingine kutokana na hofu ya kukipoteza kiumbe kinachoonekana mbeleni mwangu.
Kila kiungo changu kikawa kinafanya kazi kwa namna ya ushirikiano wa ajabu.
Kiumbe kikaonekana.
Hatua za miguu yangu zikaongezeka atimaye
nikakaribia kumfikia kiumbe hicho. Hata hivyo sikuweza kufika mwisho kabisa ya
lengo langu kabla ya kupigwa na butwaa. Nikasita. Mungu wangu! nikashtuka!.
Ulikuwa mshtuko mkubwa sana kwangu. Hapo hapo nikajikuta sina namna nyingine
niende mbele au nibadili mwelekeo wangu. Hata hivyo sauti ndani yangu
ikaniambia " wewe ni mwanaume, na siku zote mwanaume husifiwa kwa ujasiri.
Onesha uanaume wako" Nikatii sauti hiyo. Nikasogea na macho yakatua kwenye
mwili wa binti mrembo. Akiwa amejilaza mahali hapo huku macho yake yakiwa
yamefichwa na miwani mikubwa ya urembo ambayo siku hizi vijana wengi wanapenda
kuyatumia. Bado nywele zake zikawa kama zinakaribia kugusa ardhi. Ardhi hisiyo na
huruma, ardhi iliyomeza miili ya binadamu wengi. Ndipo nilipomtambua.
Nikamtambua kiumbe huyo na haraka nikaanza
kurudisha kumbukumbu zangu nyuma. Ndio! Ni binti yule ambaye niliwahi kumgonga
kule Posta. Duh! . Ni wakati huo huo binti nae akivua miwani yake na kubakia
akinishangaa. Sikuwa nafahamu kwanini alikuwa ananishangaa? Nikaanza kujiuliza
amenionaje mimi, ni kwamba sistahili kuwa hapa au ameshtushwa uwepo wangu
mahali hapa?. Mwisho nikajiona mpuuzi kuwaza vitu ambavyo sikuwa na uhakika
navyo. Nikajikuta namsalimia kiumbe huyo. Jibu lake lilikuwa tofauti na
nilivyofikiria.
Nilifikiri hasingeweza kupokea salamu yangu.
Alinijibu kwa upole na huku akinisindikiza na tabasamu zuri lililonifanya
nibabaike kidogo. Niliomba kujumika nae mahali hapo kama hatajali. Jibu lake
lilinishangaza pia, hakika hakuwa na hiana hata kidogo alinikaribisha kwa
uchangamfu wa aina yake. Nilivuta kiti ambacho hakikuwa mbali na eneo hilo.
Tukazungumza.
Tulizungumza mambo mengi sana. Ni wakati wa
mazungumzo hayo ndipo nilipouona uzuri maradufu wa binti huyo ambaye
alinikumbusha jina lake kuwa anaitwa Tayana, Tayana Masenga. Hakika siku zote
nilitambua ya wazi ni msichana mrembo. Hata hivyo sasa ndio nagundua ni
msichana mrembo zaidi kuliko nilivyofikiri, zaidi nilivyomuona mbali kwa mara
ya kwanza. Ni mrembo hasa. Alikuwa msichana anayeonekana ana akili nyingi huku
akiwa ni mwanamke mwenye kujiamini. Nikagundua pia ni mwanamke anayejua nini
anachokifanya. Tukaendelea kuzungumza.
Ni katika mazungumzo hayo ndipo alipoonekana
kushtushwa na mabadiliko makubwa niliyonayo. Kiukweli tangu niajiriwe
nilibadilika sana. Hata mwili ulianza kujiachia. Huwezi kuniweka kwenye kundi
la wanene na pia huwezi kuniweka kwenye kundi la watu wembamba. Nilikuwa mtu
mwenye mwili wa wastani. Hakika hakutegemea kunikuta mahali hapo ila kwa kauli
yake aliamini kuwa siku moja tutaonana. Nilimuuliza kwanini yupo pale?
Alinijibu kuwa yupo pale kwa ajili ya likizo yake ambayo kampuni ilimpa kwa
ajili ya kupunguza mawazo. Ni hapo ndipo nilijawa na udadisi wa kujua kipi
kilimsibu mpaka apewe likizo ya kuondoa "stress'' Maana si kazi rahisi
hata kidogo.
******************
ITAENDELEA