KARIBU USOME HADITHI NZURI ZA KUSISIMUA

SIMULIZI: Sitasahu sehemu ya Tisa (9)


hadithi nzuri ya kusisimua
Wiki moja sasa tangu nihamie nyumbani kwangu. Siku hiyo nilikuwa ofisini wakati nilipotembelewa na mgeni bila kutarajia. Nakumbuka ilikuwa mida ya saa tano asubuhi wakati katibu muhtasi wangu alipoingia na kuniambia nina mgeni anayehitaji kuniona nami... je amruhusu kuingia? Kwa sababu siku hiyo nilimwambia katibu muhtasari nahitaji muda mwingi wa kuwa busy na kazi hivyo hasimruhusu mgeni yoyote hasiye wa kampuni kuniona. 

Nina hakika kwa siku hiyo alitelekeza hilo lakini ilionekana mgeni huyu alikuwa mbishi sana kukubali kuondoka bila kuonana nami. Alisisitiza lazima aonane nami hata pale alipoulizwa je ana miadi ya kuonana na mimi? Mgeni yule alikataa na alihitaji kuonana na mimi kwa dharura.


Bila shaka niliruhusu katibu wangu amruhusu mgeni huyo kuingia ofisini. Ni wakati huo macho yangu yalikuwa yameukazia mlango huku nikijawa na shauku ya kumfahamu mgeni huyo mkorofi hasiyeheshimu kanuni za ofisi. Nilitaka kumuona kwa hamu kubwa macho yangu yakaendelea kuuelekea mlango kwa umakini mkubwa. Ndipo niliposhikwa na butwaa kwa kutoamini ninachokiona mbele yangu. Alikuwa Tayana akiwa ndani ya gauni zuri yenye rangi ya pink iliyomkaa vema mwilini.

Bila kutarajia macho ya Tayana yalitembea maili nyingi na kusambaa kwa kasi ya ajabu na niliyashuhudia yakitua kwenye kibao kilicho mbele ya meza yangu. Kibao kilinitambulisha "Manager Richard Kamba" Ni wakati ambapo macho ya Tayana yakionesha mshangao mkubwa kama mtu hasiye amini kitu anachokiona mbele yake . Nikamuachia tabasamu mwanana na kumkaribisha ofisini kwangu. Ni wakati alipokaa ndipo nilipogundua amepoteza hali ya kujiamini mbele yangu ni kama amepigwa na bumbuwazi . 

Haraka nilitambua kwanini yupo katika hali ile? Siku zote alinifahamu kama mfanyakazi wa kawaida tu katika shirika hili mpaka muda mchache uliopita ndipo alipotambua hilo hivyo kuja kwake ghafla ofisini na kunikuta mimi ndio meneja wa shirika hili ilibidi ajiulize maswali mengi zaidi bila kupata jibu.

Baada ya maongezi madogo alinieleza wazi hakupanga kuja hapa lakini ilitokea dharura kuja eneo la ofisi yetu akaonelea ni vizuri kunifanyia "suprise" kuja ofisini kwangu na alipata shida sana kufika hapa kwa sababu naliniulizia kama mfanyakazi wa kawaida lakini wote walisema hakuna mfanyakazi mwenye jina hilo zaidi ya meneja wa shirika. 

"Nikajikuta nafadhaika lakini nafsi yangu ilikuwa ngumu kukubali kushindwa ndipo nilipohitaji kumuona meneja huyo mwenye jina la mtu aliyeniambia anafanya kazi hapa. Nilipokuona wewe ndio meneja wa ofisi hii hakika nilipigwa na butwaa ni kama nisiyeamini kitu".

Maelezo ya Tayana yalinifanya nitabasamu kisha kwa mara ya kwanza nilimuomba nimpe mwaliko wa kunitembelea nyumbani kwangu wikiendi inayokuja. Nilimwambia hapo ofisini si mahali sahihi kuzungumza mambo mengi kati yetu ambayo si ya ofisi. Alinielewa huku akinisindikiza na tabasamu....tabasamu la kihisia! Tabasamu lenye kutuma ujumbe fulani mahususi....Nikang'amua anachomaanisha. Nilimuomba tukutane siku tatu baadae nyumbani kwangu.

=============================================================
Kwa muda wa zaidi ya miezi mitatu tangu nilipoanza kumfahamu Tayana niligundua vitu gani anavipenda na mambo yapi hayapendi hata kwenye vyakula pia niligundua vyakula anavyovipenda. Siku hiyo ya jumapili nilitayarisha chakula anachokipenda Tayana, chakula hicho nilikiandaa kwa mikono yangu mwenyewe. Binafsi mimi ni mpishi hodari sana jikoni na siku zote nilipenda kupika mwenyewe. Saa sita kamili mchana Tayana aliwasili nyumbani kwangu baada ya kumuelekeza .


Alikuja na gari yake mwenyewe moja kati ya magari yake ya kifahari niliyowahi kuyakuta nyumbani kwake. Alishuka garini taratibu kama malaika fulani hivi ....hakika nakiri Tayana alipendeza sana siku hiyo...uzuri wake uliongezeka maradufu ndani ya gauni fupi lenye rangi nyekundu...Gauni la kisasa ambalo lilivaliwa ndani ya mwili wa msichana mrembo wa kisasa. 

Sikujali sana. Nilipenda alivyovaa alikuwa "amazing". Kwa mara ya kwanza mimi na Tayana alikuwa ananitembelea nyumbani kwangu, tukasalimiana kisha nikamkaribisha ndani mwangu. Ndani ya nyumba iliyopuliziwa marashi yenye harufu nzuri ya kunukia.Marashi anayoyapenda Tayana siku zote kuyatumia. Niliifanya siku hiyo kuwa maalumu kwa Tayana. Ndivyo nilivyotegemea.

Tulizungumza mengi na Tayana siku hiyo. Aliniuliza mahusiano yangu ya kimapenzi yalivyo. Tangu tulipoanza kuwa karibu hakuwahi nigusia jambo lolote linalohusiana na mapenzi lakini siku hiyo aliniuliza. Jambo hilo katu sikushtuka kwa sababu nililitegemea. 

Nilimueleza wazi kutokuwa na mahusiano ya kimapenzi kwa sasa hasa chuki yangu kwa wanawake. Alinishangaa sana kwa kutoamini ninachomueleza. Aliniuliza kwa nini nawachukia wanawake? Ilinilazimu nimueleze Tayana bila kuficha ili apate kunielewa...Nikamueleza....

"Nilikuwa na mwanamke niliyempenda sana wakati ningali chuoni ni baada ya kuwa marafiki tulijikuta tukianzisha uhusiano wa kimapenzi, kila mara alikuwa akiniambia ananipenda sana. Na mapenzi yangu kwake niliyaamini. Na Nilimuamini zaidi aliponiambia anahitaji kujenga familia na mimi. 

Siku zote nilijenga matumaini makubwa juu yake. Miaka yote mitatu chuoni ilikuwa ya kusisimua sana kati yangu mimi na yeye, marafiki na wanafunzi wenzetu walituchukulia kama mfano mzuri wa mahusiano yao.

Nikajikuta nawekeza pendo langu ndani yake. Ni baada ya kuhitimu masomo yetu, haraka yeye alipata bahati ya kuajiriwa mapema nami ikanibidi nisote kutafuta kazi kwa muda mrefu...ni kipindi ambacho mpenzi wangu alipobadilika sana kitabia hasa baada ya kupata kazi akaanza dharau juu yangu. Miezi miwili baadaye alinitumia ujumbe kwenye simu yangu kuwa mahusiano yangu mimi na yeye yafikie tamati, aliniomba msamaha kwa kunipotezea muda wangu mwingi pia alinieleza wazi sikuwa mwanaume wa ndoto yake. 

Kwangu mimi alikuwa nami ili kupoteza muda na sasa amepata mwanaume wa ndoto yake. Alinieleza anatamani kubadilisha historia kati yangu mimi na yeye....anajutia uamuzi wake wa kuwa nami kimapenzi. Maneno yake yakaniumiza sana siku hiyo ilikuwa ghafla bila kutarajia...Mvulana mimi nikachanganyikiwa"

Jambo moja ambalo nililiamini.....Kila jambo hutokea kwa sababu, hili pia lilikuwa sababu. Sikutaka kupigania pendo langu kwake kwa sababu aliniambia ukweli..ukweli wenye kuumiza. Tangu wakati huo nilianza kuwachukia wanawake sikuwa na hamu tena ya viumbe hao. Niliyapigania maisha yangu kwanza.Lakini pia sikuweza kumsahau msichana huyo.

Kwa ufupi nilimaliza kumuelezea Tayana mahusiano yangu yaliyopita.Muda wote Tayana alikuwa kimya akinisikiliza huku akiniangalia usoni kutambua ukweli wangu.Bila kutarajia....Nilimuona akinifuata mahali nilipo...nami nikasimama.....ujasiri umemuingia wakati huo Tayana.

ITAENDELEA

Powered by Blogger.