KARIBU USOME HADITHI NZURI ZA KUSISIMUA

SIMULIZI: Sitasahu sehemu ya tano (5)

Pin by Larry Plummer on Eyes | Tears in eyes, Tears photography ...
Uwezo wangu wa kufanya kazi bila kuchoka, ushirikiano wangu na wafanyakazi wenzangu uliwavutia wakuu wangu wa kazi. Hivyo nikajikuta nakuwa mwakilishi mzuri wa shirika sehemu mbali mbali ndani na nje ya nchi kwa muda mfupi. Kote huko nilipopitia shirika lilikuwa likipata sifa kubwa kupitia mimi. Nikafarijika sana na kuendelea kufanya kazi kwa bidii zaidi. Jambo nisilotegemea likatokea!

Ni miaka miwili baadae yaani miaka miwili na miezi sita tangu niajiriwe kwenye shirika hili. Tukapata msiba mzito wa kuondokewa na Meneja wa shirika kwa upande wa Tanzania. Kifo cha meneja huyu kilikuja baada ya kupata ajali ya gari maeneo ya Tazara wakati huo akielekea nyumbani kwake Tuangoma -Mbagara. Ilikuwa pigo na huzuni kubwa kwa shirika na wafanyakazi ofisini hapo. 

Nakiri kwa muda mchache niliyomfahamu meneja huyu nilijifunza mambo mengi hasa ukarimu na busara zake bila kusahau ucha Mungu wake. Baada ya kumalizika shughuli nzima ya mazishi ya meneja wetu maana niliteuliwa na shirika kusimamia msiba huo. Wiki moja baadae nikaripoti kazini.

Niliwasili jumatatu ya asubuhi kama kawaida yangu na baada ya kuwasalimia wafanyakazi wenzangu nilielekea ofisini kwangu. Hata hivyo nilijikuta nikiwa na maswali mengi baada ya secretary wa ofisi ya meneja kunichangamkia kusiko kawaida huku akinitizama kwa tabasamu fulani lenye kumaanisha kuna jambo muhimu angependa kuniambia. Wakati huo bado miguu yangu na akili yangu nilishavielekeza kuelekea ofisini mwangu.

Niliingia ofisini mle kama ilivyo kawaida, macho yangu yakatua vema juu ya meza ya ofisi yangu na kuiona bahasha ikiwa imeandikwa jina langu, bahasha hisiyo ya kawaida kimuonekano. Nilikuwa napokea bahasha nyingi lakini hii ilikuwa tofauti, muonekano wake ulinisisimua . 

Nilishtuka sana, na kwa kasi ya ajabu haraka niliifungua barua ile na kuisoma kwa muda ule ule huku ningali nimesimama. "Mungu wangu!" Nilijikuta natoa sauti hafifu huku nimepigwa na butwaa. Mle ndani ya barua ile ambayo nimeisoma ilieleza imetoka makao makuu ya shirika likitoa taarifa ya kuteuliwa kwangu kuwa meneja mpya wa shirika la ndege la Ethiopia Airline. 

Kila kitu kilikuwa kama tamthilliya fulani ya kifilipino, nikajihisi kama nipo ndotoni. Nilifumba macho na kufumbua tena bado macho na akili yangu iliniambia kuwa sio ndoto. Ni ukweli halisi. Nikapagawa!

Uteuzi wangu ulienda sambamba na kupewa likizo yenye malipo ya wiki moja, kujiandaa na nafasi mpya ya umeneja ofisini hapo. Likizo yangu iliandikwa inaanza siku hiyo hiyo. Nikajikuta natoka nje kama mwehu. Kila mmoja miongoni mwa wafanyakazi wenzangu walikuwa wakinipa hongera kwa uteuzi wangu. Bado nilihisi nimo ndotoni.Ndoto nisiyotarajia. Nikajikuta najikana mwenyewe kusiko tarajiwa. Hapana sio mimi Richard. Nikarejea kuisoma upya bado jina lililomo kwenye barua hiyo lilikuwa langu. Bila shaka ni mimi niliyekusudiwa.

Nilianza kujiuliza kama nastahili cheo hiki?, wakati wapo wafanyakazi wa muda mrefu kuliko mimi. Kitu gani uongozi wamekiona toka kwangu hadi kufikia kustahili kupewa nafasi hii kubwa kabisa katika shirika? Maswali yangu kwa wakati huo hayakuwa na majibu katika kichwa changu. Nikaazimia kufanya kazi ambayo itawashangaza hata wakuu wangu. Kazi itakayokuwa na faida kubwa kwa shirika hili. Moyoni nikakubali uteuzi huo.

*************
ITAENDELEA

Powered by Blogger.