KARIBU USOME HADITHI NZURI ZA KUSISIMUA

SIMULIZI: Sitasahu sehemu ya Sita (6)

Pin by Larry Plummer on Eyes | Tears in eyes, Tears photography ...
Ni baada ya kupata kazi ndipo nilichukua jukumu la kulea wazazi wangu, ulikuwa mzigo ambao katu sikuweza kuepa. Nikabeba majukumu. Majukumu niliyostahili kuyabeba. Haraka nilimsimamisha Baba na Mama yangu kulima kwa kutumia jembe la mkono, kisha nikawa naweka vibarua huku wao wakibakia kuwa wasimamizi tu. 

Pia nililazimika kuwawekea msichana ambaye muda mwingi atakuwa anawasaidia kwa kazi za pale nyumbani. Kila mwezi nilituma kiasi fulani cha pesa kwa ajili ya kununulia mahitaji ya hapo nyumbani. Wazazi wangu walifurahi sana na kila mara walikuwa hawachoki kuniombea mimi mtoto wao.

Pengine, ushirikiano wangu na upendo wangu kwa kila mtu pale kazini uliwavutia sana wakuu wangu,nilijiambia. Hata pia utendaji wangu kazini ulikuwa wa hali ya juu na hata kufikia kupata tuzo ya mfanyakazi bora wa shirika kwa miaka miwili mfululizo. Karibu wafanyakazi wengi pale ofisini walikuwa wakinipenda na kuwa karibu nami. 

Na hata aliyekuwa Meneja mkuu hayati mzee Johnson Ndeluma alikuwa ananipenda sana na siku zote alikuwa anapeleka ripoti kuhusu mimi makao makuu. Hapo ndipo maswali yangu ya kuteuliwa kwangu kuwa meneja mkuu wa shirika kwa upande wa Tanzania yalipopata majibu katika wakati sahihi. Nikatabasamu!

Baada ya kumaliza kila kitu na kukabidhi ofisi kwa mtu atakayekaimu nafasi yangu mpaka pale nitakapomaliza likizo yangu kisha kukabishi nyaraka za kitengo nilichokuwa mwanzo kwa msaidizi wangu wa kazi kama barua ile ilivyoeleza. Msaidizi wangu moja kwa moja anaenda kuwa ofisa wa IT ofisini hapo. Kila kitu nilikifanya kwa haraka kisha niliwasha gari yangu na kuelekea katika ufukwe wa Coco ulioko katikati ya jiji la Dar Es salaam ili angalau nipunge upepo na kufurahia kuwaona watoto waliotoka katika maisha ya tofauti wakijimwaga kwenye ufukwe huo.

Ufukwe wa Coco nilitokea kuupenda sana kwa sababu nilihisi ni sehemu sahihi kwa mtu mwenye msongo wa mawazo kufika hapo. Maana kila makundi ya watu hufika hapo tofauti na fukwe zingine ambazo huwezi kuingia mpaka ulipe kiingilio. Ufukwe huu ni bure na watu wa kila aina wanapatikana hapo.

Niliwasili katika ufukwe huo mida ya mchana, sikumbuki ilikuwa saa ngapi bali ilikuwa kati ya saa saba hadi saa nane mchana. Nikakijongea kiti cha plastic na kukaa hapo nje ya mgahawa na kuagiza kinywaji huku nikiwatizama vijana kwa watoto wakiogelea. Nilijisikia raha sana na kukumbuka nyakati nyingi zilizopita.

Wakati huo nilipokuwa mwanafunzi kule Tukuyu na kipindi fulani tulikuwa tunakwenda Matema beach kujivinjari. Kumbuka mpaka wakati huo sikuwa na mahusiano na msichana yoyote. Hata wale wafanyakazi wa kike waliokuwa wakijigonga ofisini waliishia njiani. Ilifikia hadi kupewa kashfa kuwa mie Jogoo halipandi mtungi. Binafsi sikujali kwa sababu niliufahamu ukweli.

Vile vile sikuwa mnywaji wa kilevi chochote na sikuwa mvutaji pia. Kinywaji changu pekee ni juice na soda tu. Baadhi ya marafiki zangu walikuwa wananidhihaki kwa kuniambia mie bado mshamba tu kwa sababu situmii kilevi kama wao. Nalo pia sikujali sana kwa upande wangu Kwa sababu kitu kimoja nilichokuwa nacho ni kusimamia kile ninachokiamini. Hicho ndicho kilichokuwa kinanisaidia.

Wakati nipo hapo Coco beach nikawaza sana na kisha nikajiambia likizo hii ya wiki moja yanipasa niende kuitumia Tukuyu pamoja na wazazi wangu ambako toka nilipohitimu chuo kikuu sikuwahi kwenda au niende sehemu nyingine nje ya Dar es Salaam?. Nikawaza sana. Wakati naendelea kuwaza jina la Zanzibari likapita kichwani mwangu. Ni hapo sauti mbili zikaanza kushindana na akili yangu katika maamuzi.

Upande mmoja ukaniambia ukienda Tukuyu ni sehemu sahihi zaidi kwako kwa sababu Baba na mama yako wana hamu kubwa ya kukuona. Na upande mwingine sauti ikanitaka nipuuze kwenda Tukuyu, na ikinitaka kuwa niende katika kisiwa cha Unguja kilichopo Zanzibari. Huko nitafurahia sana wakati wangu alafu pia kwenda Tukuyu ni vizuri niende na mchumba kumtambulisha. Sauti hizi mbili zikanifanya nibakie njia panda nisijue wapi ni sahihi zaidi. Mwishowe niliazimia kwenda Tukuyu mkoani Mbeya kuwaona wazazi wangu.

Baada ya kutosheka mahali hapo nikawasha gari na kurejea nyumbani kwangu Mbezi ya Kimara mahali ambako ndipo nilipopanga. Usiku huo kwangu ulikuwa mgumu sana, bado sauti ya kunishawishi nibatilishe uamuzi wangu wa kwenda Tukuyu na kisha niende Zanzibar haukukoma. Kila muda ulivyokuwa unakwenda ndivyo nikajikuta naanza kushindwa kuutetea uamuzi wangu nilioufanya kabla...Uamuzi wa kwenda Tukuyu. Sasa akili ikatawaliwa na kwenda Zanzibari.

Bila kutambua nikajikuta nawasha Laptop yangu ndogo na kuitafuta Zanzibar. Nikaanza kuona uzuri na mambo mengi yakaanza kunivutia.Simulizi za marafiki zangu ningali chuoni hasa kwa vijana wale watokao huko visiwani vikanifanya niufikirie mara mbili uamuzi wa kwenda Tukuyu haukuwa uamuzi sahihi. Bila ajizi nikabadili safari ya Tukuyu huku nikikubali ushauri wa kuwa nitaenda huko nikipata mchumba ili wazazi wangu wafurahi. Nikaamua niende Zanzibar. Ni Zanzibari ndipo historia yangu ikabadilika.

Baada ya kufikia makubaliano na akili yangu, na kuazimia kwenda Zanzibari. Usiku huo huo nikajikuta nikivutiwa na Hoteli ya MELIA iliyopo Zanzibar tena ni baada ya kusoma tangazo lao kwenye Gazeti siku chache zilizopita na usiku huo nikajikuta naitafuta hoteli hiyo kwenye mtandao. Ilionekana ni Hoteli nzuri kwa upande wangu. Nikachukua mawasiliano yao na kuongea nao usiku huo huo.

INAENDELEA


Powered by Blogger.