SIMULIZI: Penzi La Mfungwa sehemu Ya Ishirini na Moja (21)
Kabla Mr Rasi hajafika ile sehemu waliyomuacha Zabroni, Zabroni machale yalimcheza akaamua kuondoka mahali hapo haraka sana akiamini kwamba tayari Tina ndio mtu pekee mwenye uwezo wa kuvujisha siri ambayo ingeliweza kumtia hatiani akashindwa kulipa kisasi.
Hivyo wakati Mr Rasi anafika na gari yake hakumkuta Zabroni, aliumia sana kwa maana alijua hiyo ndiyo nafasi ya kumuangamiza adui yake.
Zabroni sasa alianza kuhofia usalama wake,na hapo aliamua kutoka nje ya jiji la Dar es salam. Akaenda pembezoni mwa jiji ambapo huko alianzisha makazi yake mapya, aliachana na ile style ya kuwa mzoa takataka.
Huko kando ya jiji alikaa takribani miaka mitatu kiasi kwamba hata wale Askari waliopewa majukumu ya kumsaka mfungwa huyo walianza kukata tamaa. Lakini mara baada kupita miaka hiyo mitatu,hatimaye alirudi tena mjini. Alijikita katika kazi ya kuosha magari huku umakini ukitawala ipasavyo katika mwili wake. Safari hiyo alibadilisha jina akajiita Ramso.
Siku moja hapo car wash ilikuja gari ndogo aina ya Noah,ndani ya gari hiyo alishuka binti mrembo. Binti huyo aliitwa Lina.
Lina aliposhuka kwenye gari alichomoa simu kwenye mkoba wake,akawa amedondisha fedha shilling elfu tharathini zikiwa zimekunjwa. Bila kujua kama kadondosha fedha hizo alimsogelea Zabroni,kwani yeye tu aliyeonekana hana kazi muda huo. Alimsalimia kisha akamwambia amuoshee gari yake,Zabroni ambaye ni Ramso alimtajia bei. Lina hakuteteleka zaidi kusema "Haina tabu,basi naomba unioshee haraka nakuja mara moja.
Nikitoka huku nikute umemaliza sawa kaka?..",alisema Lina msichana mrembo kuliko hata jina lenyewe. "Sawa ",alijibu Zabroni kisha mara moja akaanza kazi huku Lina naye akiambaa ng 'ambo ya barabara ambapo mbele kidogo palikuwa na jengo la supermarket. "Watu na maisha yao",alisema Zabroni wakati huo ameshaanza kuiosha gari la huyo mwanadada atwae Lina. Alipokaribia kumaliza, mara ghafla akaziona zile fedha alizodondosha Lina.
Hima aliziokota akazitia mfukoni kisha akaendelea kuosha gari hadi akamaliza ambapo alikaa pembeni kusubiri ujira wake. Baada ya nusu saa Lina alirejea huku macho yake yakionekana kutazama chini wakati wote kana kwamba kuna kitu anakitafuta,alipomkaribia Zabroni alimlipa ujira wake kisha akapanda Kwenye gari.
Kabla hajaondoka, Zabroni alimfuata kisha akatoa mfukoni zile fedha akamkabidhi "Dada hizi pesa zako? ..",Lina baada kuziona alishusha pumzi kwa kask kisha akajibu "Ndio..Doh! Nimezitafuta sana...kiukweli ni watu wachache sana wenye moyo kama wako. Kaka hebu nambie unaitwa nani?.."
Naitwa Rasmo",alijibu Zabroni huku Lina akimtazama usoni bila kupepesa macho.
Alimshukuru sana,alichukuwa shilling elfu kumi tu zilizobaki akamwachia mtukutuku Zabroni. Na tangu siku hiyo mazoea yakaanza baina ya Zabroni na Lina. Mazoea hayo mwishowe yakazaa mahusiano,ambapo baada mahusiano kukolea,Lina alimtaka ampeleke mpenzi wake akamtambulishe kwa wazazi wake. Wakati huo baba yake Lina ni Afande Jimmy, moja ya maafande aliyepewa jukumu la kumtafuta Zabroni ambaye tayari ni mpenzi wa mwanaye.
Mpaka nyumbani kwao na Lina Zabroni alifika,alimkuta mama yake sebuleni huku baba Lina akiwa chumbani. "Mama nafikiri niliwahi kuwaambia kwamba nimepata mchumba",alisema Lina kwa sauti ya kusitasita.
"Ndio mwanangu nakumbuka,na bahati nzuri leo baba yako hajaenda kazini. Yupo ndani kapumzika,basi ngoja nimuite",alijibu mama Lina kisha akasimama akazipiga hatua kuingia chumbani huku sura ya huyo mtu aliyekuja na mwanaye ikimjia kwa mbaali kichwani mwake.
Punde si punde baba yake Lina Afande Jimmy alitii wito,alipokaa kwenye sofa tu macho yake yakagongana na uso wa Zabroni ghafla alishtuka, akakumbuka kuwa huyo ni mfungwa anayesakwa kwa udi na uvumba. Vile vile dau nono litatolewa kwa kamanda ambaye atafanikisha kumtia mbaloni.
Alistuka Afande Jimmy, ilihari muda huo Zabroni naye akionekana kutaharuki baada kugundua kuwa tayari yupo mkononi mwa Askari magereza aliyekuwa akimlinda jela. Pumzi kwa nguvu alishusha,huku akifikiria ni vipi atang'atuka hapo kibindoni. Wakati huo Jimmy alinyanyuka kutoka kwenye sofa akarudi chumbani upesi kisha akamuita mkewe "Mama Lina hebu njoo mara moja ",bila kuchelewa mama Lina alinyanyuka akamfuata chumbani mumewe huku subuleni presha ikizidi kumpanda Zabroni kiasi kwamba mpaka Lina alitambua kwamba Zabroni hayupo sawa huo muda ingawa hakutaka kumwambia.
Chumbani kule, Jimmy alimwabia mkewe ukweli kuhusu kijana Zabroni kitendo ambacho kilimfanya mama Lina naye kuvuta kumbukumbu,alikumbuka siku kadhaa zilizo pita "Kwa kumbukumbu zangu kiukweli huyu mwanaume sio mgeni machoni mwangu. Namkumbuka vizuri sana ila siku hiyo nilipomuona alionekana anafanya kazi ya kuzoa takataka.
Lakini pia kwenye maongezi niliyokuwa naongea naye alinambia kwamba alisoma na Veronica, yule Vero mtoto wa mzee Busere ambaye kwa sasa ni Askari. Kwahiyo unapo niambia kwamba huyu katoroka jela,dah.
Unanichanganya kidogo kiukweli ",alisema mama Lina. Jimmy alitazama paa la nyumba akionekana kutafakari kitu fulani akilini mwake,akashusha uso wake chini wakati huo akishusha pumzi ndefu. Baada ya hapo alisema "Unajua kwamba endapo kama nitamkamata huyu mtuhumiwa tutaogolea mapesa? Lakini pia hataakama ni mkwe wetu,huyu Lina bado anatakiwa aendelee na masomo sasa iweje atuletee masuala ya uchumba?
..hapana siwezi kukosa pesa,vile vile siwezi kuepuka kupandishwa cheo wakati mtuhumiwa tayari yupo mikononi mwangu..", aling'aka kamanda Jimmy kisha haraka sana alisogelea droo ndogo ya kitanda, akatoa pingu na bastora. Hima alirudi sebuleni ambapo alimkuta Zabroni na Lina wakiongea mambo kadhaa wa kadha huku Lina akionekana kumtoa wasi wasi Zabroni. "Kijana hapo hapo ulipo hebu simama juu na unyooshe mikono yako..", kamanda Jimmy alitoa amri hiyo huku akimnyooshea bastora Zabroni.
Lina alistuka akajikuta haelewi kinachoendelea,kwani yeye hakufahamu kwamba mpenzi wake ni mfungwa aliyetoroka gerezani. "Baba nini sasa unataka kufanya? Kwanini unamtisha kijana wa wawatu? Ama mimi sistahiri kuwa na mwanaume?..",alihoji Lina huku akilia,lakini kilio chake katu hakikuweza kumfanya mzee wake ashindwe kutimiza agizo lake alilotumwa. Alimvisha pingu mkononi Zabroni, moyoni akiwa amedhamilia kumrudisha Zabroni jela.
Hapo sasa Lina alimsogelea baba yake kisha akamshika mkono ili asifanye uamuzi huo, kitendo hicho kilimkera sana Afande Jimmy ambapo alimpiga kofi binti yake na kisha kumtupia maneno makali. Lina akaangukia kwenye sofa ilihari muda huo huo Jimmy alimuongoza Zabroni mbele yeye nyuma tayari kwa niaba ya kumpeleka moja kwa moja sehemu husika.
Lakini kabla hajampandisha kwenye gari lake,ghafla alisikia sauti ya ya Lina ikimuita. Afande Jimmy aligeuka akajikuta akistuka baada kumuona Lina akiwa ameshika kisu kwa dhumuni la kutaka kujiuwa. Machozi yakimtiririka akasema kwa uchungu "Baba,endapo utaitosa furaha yangu. Basi na mimi najiuwa hapa hapa mbele yako. " Kwisha kusema hayo alianza kujihesabia namba.
Wakati huo mama Lina naye upande wa pili alikuwa akilia huku akimsihi mumewe asimrudishe Zabroni Jela, amuache huru kwani kufanya hivyo itapelekea kumkosa mtoto wao pekee, ambaye ni kama mboni yao.
Hapo Jimmy hakuwa na namna tena,alichomoa funguo ya pingu. Akamfungua Zabroni ingawa moyoni akionekana kufura hasira. "Huu ni upuuzi kabisa,kweli bora uzae chura kuliko mtoto wa kike mpumbavu kama huyu alaah ",alisema Afande Jimmy huku akizipiga hatua kurudi ndani ilihari muda huo Lina alidondosha kisu chini kisha akamsogelea Zabroni na kumkumbatia.
Basi mapenzi ya watu hao wawili yaliendelea kushamili,kiasi kwamba ilimpelekea Zabroni kumsahau kabisa Tina. Siri kuu aliitunza Afande Jimmy kwani tayari mtuhumiwa yupo kwenye mji wake.
Lakini mwishowe aliona kuishi na Zabroni nyumbani kwake ni jambo la hatari sana kwa kibarua chake kwa maana tayari Zabroni ni mtu anayetafutwa na serikali mahali popote pale,hivyo endapo kama atabainika kuwa yupo nyumbani kwake basi huwenda Jimmy akatuhimiwa kumtorosha mfungwa huyo kitendo ambacho kitaweza kumfukuzisha kazi lakini pia hata kuhukumiwa kwa kosa hilo la jinai.
Hivyo Jimmy alimtafutia Zabroni nyumba nyingine mbali na eneo hilo analo ishi yeye. Huko alimpangishia chumba pia alimkabidhi gari ya kutembelea huku akimsisitiza umakini wa kuishi maisha hayo ya wasiwasi kuhofia kurudishwa jela.
Hakika lilikuwa ni jambo la furaha sana kwa Lina baada kuona baba yake ameendana na matakwa yake,hicho ndicho alichukuwa anakitamani kije kutokea. Kweli hatimaye siku hiyo kikaja tokea asijue ya kwamba kijana huyo licha ya kuwa naye kwenye mahusiano lakini pia anamkakati mzito sana wa kulipa kisasi.
Hivyo kukabidhiwa kwake usafiri binafsi kulimfanya aanze kutembembea maeneo mbali mbali ndani ya jiji huku akitamani walau siku moja akumbane na Veronica,ila bahati mbaya haikuweza kutokea siku hiyo. Upande wa pili,Mr Rasi alijikuta akikosa amani wakati wote baada kugundua kuwa adui yake yupo naye ndani ya jiji.
Aliwaza ni wapi atambamba ili amalizane naye kibingwa? Ikiwa wakati huo Zabroni naye akiwaza ni wapi atakumbana na Veronica amalizane naye asitambue ya kwamba Mr Rasi ama Bruno naye yupo jijini anamtamani kama mlevi aonapo pombe.
Siku zilisonga, miezi ikasogea. Mr Rasi akiendeleza kichapo kwenye mapigano yake huku Lina naye akiendelea kumtunza mpenzi wake hasa kujitahidi kutunza siri baada kujua kuwa mpenzi wake ni mfungwa aliyetoroka jela.
Siku moja jioni sana,ilionekana gari aina ya Rav4 ikiingia nyumbani kwa kina Lina. Gari hiyo baada kupaki eneo maalumu alishuka msichana mrembo,msichana huyo hakuwa mwingine bali ni Veronica. Naam.
Veronica na Lina ni marafiki wa kufa na kupona tangu walipokuwa shule ya msingi mpaka chuo. Siku hiyo Veronica alikuja nyumbani kwa kina Lina kwa niaba ya kumsabahi rafiki yake baada kupita miaka kadhaa bila kuonana.
"Karibu sana,Veronica ",Mama Lina alimkaribisha Veronica kwa bashasha ya hali ya juuu.
"Ahsante sana mama nimekaribia" alijibu Veronica huku akiketi kwenye Sofa. Salamu zilifatia kisha mama Lina akamtania kidogo Veronica kwa kusema "Naona tangu siku ile tukutane barabarani Magomeni,hatujaonana tena..
khaa Veronica kama vile nyumbani kwangu hupajui? " alisema huku akitabasamu. Veronica akajibu "Ni kweli mama lakini nafikiri yote ni shauli ya kazi,istoshe nimehamia makazi mapya siku za hivi karibuni kwahiyo iliniwe vigumu kuanza kuzurula. Ila hakijaharibika kitu ndio nimekuja sasa...aammh kwanza Lina yuko wapi?.."
"Lina katoka tangu asubuhi,ngoja nimpigie aje haraka maana siku nyingi hamjaonana" ,Hima mama Lina alichukua simu yake akampgia binti yake. Lina akapokea ikasikika sauti ya mama yake ikisema "Lina ukowapi? Njoo nyumbani Vero kaja kukuona"
"Haaah! Vero? Mwambie nakuja anisubiri asiondoke",alijibu Lina kisha akaitupa simu kitandani akaendelea kuziweka sawa nywere zake kwani muda huo alikuwa ametoka kuoga baada kumaliza mchezo baina yake na mtukutuku Zabroni. Punde si punde Zabroni naye alionekana akitokea bafuni,lakini hakusikia kile Lina alichomjibu mama yake.
Ila wakati anajifuta maji kwa taulo,Lina alimsogelea kisha akamwambia "Mpenzi wangu Ramso,Leo nimejikuta napata furaha zaidi. Rafiki yangu kipenzi kaja nyumbani kunitembelea kwahiyo naomba ujiandae twende wote ili nikakutambulishe kwake" ,alisema Lina kwa furaha asijue ya kwamba Zabroni ambaye yeye alimfahamu kwa jina Ramso anamtafuta kwa udi na uvumba Veronica ambaye ni huyo rafiki yake kipenzi aliyekuja kumtembelea siku hiyo.
"Usijali tutaenda, pamoja", Zabroni alijibu pasipo kujua ni nani huyo anayekwenda kumuona.
Wawili hao walijiandaa haraka haraka kisha wakaanza safari;wakati huo jioni ishatoweka,giza totoro tayari lilikuwa limeshatanda ndani ya jiji la Dar es aSalaam. Walipokuwa ndani ya gari,Zabroni na mpenzi wake wakuitwa Lina walikuwa wakiongea mambo mbali mbali hasa hasa kuhusu mahusiano yao.
Lina alisema "Kiukweli Ramso sijatokea kumpenda mwanaume kama ninavyokupenda wewe,ndio maana baba alipotaka kukurudisha jela nikatishia kujiuwa "
"Ahsante sana kwa maneno yako matamu, je kwa mfano angenirudisha huko ungejiuwa kweli ama ulikuwa unamtisha tu?.."
"Kha Ramso,hakyaMungu ningejiuwa sitanii. Ujue mimi sipendi kukosa furaha katika maisha yangu. Lakini pia istoshe wazazi wangu wananipenda sana na ndio maana baba aliponiona nimeshika kisu haraka sana akakufungua pingu " alisema Lina huku akiwa amemgeukia Zabroni ambaye naye alionekana kuwa makini barabarani.