KARIBU USOME HADITHI NZURI ZA KUSISIMUA

SIMULIZI: Penzi La Mfungwa sehemu Ya Tatu (03)

simulizi ya penzi la mfungwa
Mkutano wa kijiji ulifanyika siku hiyo,waliopata taarifa ya msiba huo walifika na ambao hawakupata hawakufika. Mazishi yalifanywa na wanakijiji wachache sana, hakuna aliyekuwa na taarifa kuhusu msiba huo, mjumbe wala mwenyekiti hawakufika pia. Jambo hilo lilimuumiza sana mzee Maboso akajiaminisha kuwa huwenda vifo hivyo ukawepo mkono wa mtu. Wakati mzee Maboso akiwaza suala hilo upande wa Zabro naye aliamini kama mzee Maboso alivyokuwa akiamini.

Baada ya msiba, mzee Maboso akamtaka Zabroni aishi nyumbani kwake, lilikuwa pigo baya sana katika maisha yake. Jambo hilo liliweza kumfanya asitishe zoezi la kuendelea kuiba, kwani aliyekuwa akimfanya aibe ameshapoteza maisha. Lakini licha ya kuamua kuacha zoezi hilo, ndani ya moyo wake kuna kitu alipania kukifanya mbadala. Roho ilimuuma sana, aliona hatolizika endapo kama kitu hicho hatokitekeleza 

"Nitahakikisha kila siku iendayo kwa Mungu nyumba moja inateketea kwa moto", alijisemea kwa uchungu ndani ya nafsi yake Zabroni, chozi halikusita kutiririka kunako mboni za macho yake. Akaona uamuzi wa kuchoma nyumba kila siku iendayo kwa Mungu ni uamuzi mzuri na sahihi pia. Uamuzi huo hakutaka kuufanya pasipo kumshirikisha mzee Maboso ambapo mzee huyo alimsifu sana Zabroni kwa kuamua kuchukuwa uamuzi wa kiume. 

Akaachia tabasamu bashasha kisha akasema "Safi Zabroni, upo sahihi. Samaki mmoja akioza, wote wameoza. Ukweli nina mashaka na uongozi wa juu kwenye hiki kijiji juu ya suala hili la kuwaawa kwa wazazi wako. 

Mimi nipo nyuma yako kijana wangu. Kesho nitakupa mzizi utautafuna, ni dawa ambayo itakufanya upotee katika mazingira yoyote pindi utakapo nuia maneno ambayo nitakwambia hapo kesho. 

Natamani lengo lako litatimia Zabroni ", tabasamu bashasha lilionekana usoni kwa Zabroni kupitia mwanga hafifu wa koroboi (Kibatali), baada tabasamu hilo akajibu." Nitakushuru sana, hakika nitachoma nyumba moja baada ya nyingine usiku usio julikana "

" Naam! Jasiri haogopi ", aliunga mkono mzee Maboso kisha akamtaka Zabroni atie unga unga kwenye maji waliyonjika jikoni, wasonge ugali wale ili kesho wagange yajayo.


Kesho asubuhi palipo pambazuka,mzee Maboso ndio alikuwa wa kwanza kuamka ambapo kabla ya yote alitoka nje kujisaidia kisha akarudi ndani. Alipo ingia ndani alimuamsha Zabroni na kumwambia "Mimi naenda kukagua mitego yangu nikirudi tupukuchue mahindi ili twende nashineni sionaona unga umetuishia?.." Zabroni aliposikia hiyo sauti ya mzee Maboso, haraka sana akakurupuka kutoka usinguzini na kisha akamjibu "Usijali hii kazi niachie mimi,we nenda kaangalie mitego yako babu wala usijali "

"Sawa hamna shida ",alijibu mzee Maboso wakati huo akichukuwa panga na mkuki akaelekea porini kukagua mitego yake. Muda mchache Zabroni aliamka akanawa uso na kisha akaingia kwenye ghala kuchukuwa mahindi. Lakini kabla hajaanza kuyapukuchua,akaja Tina. Tina na Zabroni ni wapenzi, hivyo siku hiyo Tina alikuja kumuona Zabroni baada kuona muda mrefu hawajaonana na wala hana taarifa naye. 

Alifurahi sana kumuona mpenzi wake kwa mara nyingine, alizipiga hatua za kunyata ilihali Zabroni naye akionekana kuandaa mahali pakupukuchulia mahindi lakini alijikuta akizibwa macho na mtu ambaye hakumjua,ila baadaye kidogo Tina alitoa mikono yake kwenye macho ya Zabroni alicheka kidogo kisha akasema "Zasiku Tina"

"Safi Zabro,kwanza pole na matatizo. Lakini pia naomba unisamehe kwa kutokufika msibani. Wazazi walinikataza kufika mpenzi wangu", aliongea Tina kwa sauti ya chini huku akimtazama Zabroni kwa haibu Tina kwa sauti,Zabroni akamtoa shaka halafu akamjibu "Huna sababu ya kuniomba msamaha Tina,hayo ni mambo ya kawaida sana kwahiyo furahi kunikuta mzima". baada kusema hayo wawili hao waliketi chini wakaanza kupukuchua mahindi.

Wakati hayo yanajili, upande wa pili nyumbani kwa mwenyekiti alifika mzee Fungafunga. Fungafunga alionekana anamazungumzo na mwenyekiti siku hiyo ,kwa maana hiyo ilimbidi mwenyekiti aache kazi aliyokuwa akiifanya muda huo,alikuwa akitengeza mipini ya jembe. 

Sikio na mawazo yake akamkabidhi mzee Fungafunga ikamsikiliza mzee huyo ana jambo gani anataka kumwambia. Mzee Fungafunga akapewa kigoda akakaa,akakohoa kidogo kisha akaanza kusema "Naona kajua kanawaka"

"Mmh kiangazi hii bwana,kulikoni mbona leo hujaenda shamba"

"Nilikuwa namaongezi juu yako,ndio maana siku hii nimeamua iwe kwa ajili yako" alijibu mzee Fungafunga.

"Mmh sawa nakusikiliza"

"Kabla sijaingia kwenye jambo lanyewe hivi mipini huwa unatengeneza kwa shilingi ngapi?.."

"Aah bei poa tu kwa wewe elfu tatu tu"

"Anhaa. Sawa. Jambo lanyewe sasa ni kuhusu huyu kijana huyuuu.. Zabroni "

"Huyu mtoto wa marehemu mzee Ndalo? .."

"Huyo huyo,ujue tangu wazee wake wafariki tabia ya wizi imetoweka hapa kijijini"

"Kwa maana hiyo wanataka kusema yeye ndio alikuwa mwizi?". Fungafunga alikaa kimya kidogo kisha akajibu "Ndio maana yake! Au unaonaje?.." Mwenyekiti naye akakaa kimya muda mfupi halafu akajibu "Bila shaka naweza kuungana na wewe,sasa unanishauri nini?.."

"Mimi sina cha kukushauri ila nataka nikuulize swali! Vipi ukimfahamu muhusika wa tukio la kuchoma moto nyumba ya mzee Ndalo? .." mwenyekiti akashusha pumzi kwanza,akakohoa halafu akajibu "Kwa jinsi yule mzee nilivyokuwa simpendi,kiukweli nitampatia zawadi huyo muhusika. 

Unajua yule mzee tangu kipindi kile aninyime baiskeli yake nilimchukia sana na ndio maana hata msibani sikwenda,sio mimi hata balozi wangu nae hakwenda sijui wewe mwenzangu " Fungafunga aliposikia maneno hayo ya Mwenyekiti alicheka sana kisha akajibu "Wala sikwenda,kwanza mimi ndio muhusika wa tukio lile. 

Ukweli mzee Ndalo nilimuazima pesa kwa niaba ya matibabu ya mkewe lakini wakati wa malipo akaanza kunizungusha. Sikuwa na sababu nyingine mimi", Mwenyekiti alipigwa na butwaa kidogo ila mwishowe akarudi katika hali yake ambapo alikutana na Fungafunga akisema huku akianza kwa kucheka "Nipe zawadi yangu sasa"

"Baadaye tukutane kwa mama Ziada kuna ulanzi pale njoo tuburudike mzee mwenzangu kwani umekuwa shujaa ",alijibu Mwenyekiti, mzee Fungafunga akafurahi baada ya hayo akaaga na kuondoka zake nyuma akimuacha Mwenyekiti akilitafakari tukio lile huku akijiuliza kwanini baada wazazi wa Zabroni kuuwawa matukio wizi yametoweka kijiji hapo.



Kwingineko Zabroni na mpenzi wake ambaye ni Tina walikuwa wakiendelea kupukuchua mahindi,huku wakipiga zogo la hapa na pale. Baada kumaliza Tina aliaga kuwa anarudi nyumbani kwao,Zabroni aliamua kumsindikiza wakiwa njiani Zabroni akamwambia Tina "Tina najua ipo siku mimi nitafungwa jela,kwa sababu nitahitaji kulipa kisasi juu ya kifo cha wazazi wangu", Tina akastuka kusikia maneno hayo,akajibu "Unajua Zabroni mimi nimeshakuzoea,istoshe nakupenda sana. Je, unafikiri ukifungwa mimi nitakuwa katika hali gani? Hebu muachie Mungu ndio ataweza kukulipia"

"Tina dawa ya moto ni moto,acha nilipe kisasi? Lakini pia..." Kabla Zabroni hajaongea alichotaka kusema,mara ghafla mzee Fungafunga alifika. Tina ni mtoto wa mzee Fungafunga,ilihali mzee huyo ndio aliyehusika na mauaji ya wazazi wa Zabroni. 

Tina baada kumuona baba yake aliogopa sana,mara moja akatimua mbio wakati huo huo Zabroni naye aligeuka kurudi nyumbani ambapo alikutana uso kwa uso na mzee huyo. 

Mzee Fungafunga akamtazama Zabroni kwa jicho ngebe kisha akasema "Sitaki mazoea na mwanamgu mwana haramu wewe", Zabroni hakujibu neno lolote, alimtazama tu kisha akaishia zake. Lake rohoni.

INAENDELEA
Powered by Blogger.