KARIBU USOME HADITHI NZURI ZA KUSISIMUA

SIMULIZI: Penzi La Mfungwa sehemu Ya Kumi (10)

simulizi ya penzi la mfungwa
Madebe pamoja na Bruno walizipiga hatua kuelekea kwenye nyumba moja kijijini hapo wakiwa na lengo la kumuulizia Mwenyekiti wa kijiji,kwenye mji huo waliwakuta watoto. 

Watoto hao walionekana wanyonge sana hasa kutokana na mambo maovu yaliyokuwa yanaendelea hapo kijijini huku wao wakishuhudi kwa macho yao,hali hiyo ya unyonge kwa watoto iliwauma sana Madebe na Bruno lakini iliwapasa kupiga moyo konde wakawauliza watoto hao wapi walipo wazazi wao. Mtoto mmoja mkubwa kuliko wote alijibu 

"Mama na baba hawapo wameenda shamba", alijibu mtoto huyo huku akionekana kuwa na hofu,nao hao vijana baada kupata jibu hilo kutoka kwa mtoto huyo waliendelea na safari yao,ilihali macho yao yakionekana kutazama kila pande ya kijiji kutazama jinsi kijiji kilivyo chakaa majivu yaliyotokana na nyumbaa kuungua.

Hatimaye walifika kwenye nyumba ya pili,hapo waliwakuta wenye nyumba. Madebe alijitambulisha pia alimtambulisha na mdogo wake kisha wakasema nia na dhumuni ya kufika kijijini hapo,nia yao ni kusaka maisha kwa njia ya kilimo. Vile vile walisema kuwa ni vema kabla ya kuanza kazi waonane kwanza na Mwenyekiti wa kijiji ili pindi yatakapo tokea matatizo basi wajue ni jinsi gani ya kuweza kusaidiana. 

Baba mwenye nyumba hiyo aliwaelekeza mahali ilipo nyumba ya Mwenyekiti wa kijiji,Madebe na Bruno wakaelekea huko ambapo walimkuta Mwenyekiti akijenga nyumba yake ndogo baada kubwa aliyokuwa akiishi hapo wali kuungua na moto.

"Hodi hapa ", alisema Madebe,mwenyekiti alipo sikia sauti hiyo alisitisha zoezi lake la kuparata udongo pembeni kisha akageukia kule ilipotokea sauti. Aliwaona vijana wawili. Vijana hao walikuwa wageni kabisa machoni mwake. Hivyo kimoyo moyo alijisemea "Ugeni huu", wakati anasema hayo tayari hao vijana walikuwa wameshajongea Karibu yake kabisa.

"Shikamoo mzee"

"Shikamoo babu" Madebe na Bruno walimsalimia Mwenyekiti. "Malahabaa hamjambo? Karibuni sana", alijibu Mwenyekiti huku akiwasogezea benchi ili wapate kukaa. Walikaa kisha utambulisho ukafuatia,Madebe alijitambulisha pia akamtambulisha na Bruno. 

Na mwisho wa yote Madebe alieleza lengo kuu lililowafanya waje hapo kijijini,na katika malengo hayo hawakuweza kusema kama wanamikakati ya kulikomesha tatizo sugu linalo kikumba kijiji hicho.

"Karibuni sana vijana,kweli siku zote ujana ndio nafasi pekee ya kujijenga kiuchumi ili uzeeni usipate shida. Hakika nyinyi ni mfano wa kuigwa, lakini je mtapaweza hapa?..", alihoji Mwenyekiti, Madebe na Bruno walitazamana kisha Bruno akajibu "Siku zote mtaka cha uvunguni sharti ainame. 

Kwahiyo sisi tuatapewaza tu kama nyinyi wazee mnapaweza sembuse sisi? Tena vijana wanye nguvu zetu?.." Madebe naye alidakia akasema "Kwani ni sababu ipi ambayo inakutia hofu kuwa sisi hatukiwezi kijiji hiki? .." Mwemyekiti hakujibu zaidi alishusha pumzi kwanza kisha akajibu "Zabroni! Zabroni, kijana mtukutu ambaye tangu nizaliwe sijawahi kumuona kijana kama huyu. 

Hana hata chembe ya huruma,tangu wazee wake wauliwe kwa kuchomwa moto wakiwa ndani ya nyumba basi amekuwa muuaji,katili yani doh",alidondosha machozi Mwemyekiti huku akisimulia jinsi mtukutu Zabroni anavyofanya mambo ambayo binadamu wa kawaida hawezi kufanya,jambo kuu ambalo lilimuuma Mwenyekiti wakati anasimulia hayo ni kuhusu kifo cha mkewe pia na kifo cha mzee Baluguza.

"Pole sana mzee wetu lakini kuhusu hilo wewe usijali sisi tutavumilia istoshe tuna malengo na maisha yetu,mpambanaji hachoki mzee wetu" alisema Buruno.

Walipata nafasi ya kulaza mbavu zao,kesho yake asubuhi Mwenyekiti aliambatana na vijana hao mpaka nyumbani kwa muhindi,ambaye ndio tajiri wa kijiji. Hapo mwenyekiti aliamini lazima jamaa huyo atakuwa na shida na vibarua kwani ni mara chache sana shambani kwake kukaukiwa vibarua lakini kutokana na mambo yaliyokuwa yanajili kijijini hapo ikafikia hatua vibarua wakaadimika. Vibarua walipata, hekari mbili walikabidhiwa za kupalilia zao la muhogo huku hifadhi yani mahali pa kulala ikiwa ni kwa Mwenyekiti.

Kesho yake asubuhi walianza kazi,walifanya kazi huku mioyoni mwao wakiwa na lengo lao lile lile ambalo ni kumshikisha adabu mtukutu Zabroni, na lengo lao hilo waliliweka siri yao wawil pasipo kumwambia mtu yoyote.

Siku zilisonga wakiendelea kufanya vibarua, walisaidiana na Mwenyekiti kujenga nyumba kwa mapema zaid wakawa sasa wanalala ndani kwa amani kwani kipindi hicho Zabroni alikuwa ametuliza makeke yake. Miezi takribani miwili sasa ilikatika,hali ikiwa shwari kijijini hapo. Hakika ilikuwa ni jambo la furaha sana kwa wanakijiji, na hapo ndipo uvumi ulipoa anza kuzagaa kila kona ya kijiji pamoja na vijiji jirani wakivumisha kwamba Zabroni kauliwa,wengine wakisema katiwa uchizi huku wengine wakidiriki kuvumisha ya kwamba kijana huyo mtukutu kafungwa jela. 

Ila baadae uvumi huo ulikuja kuonekana si chochote si lolote baada usiku mmoja kuungua nyumba. Lakini pia usiku huo huo jeshi la polisi lilivamia kijiji hicho wakimtafuta Zabroni pasipo kujua kuwa kijana huyo anatumia dawa hakamatiki kirahisi. Jeshi hilo lilikesha likifanya dolia, kesho yake asubuhi ndipo lilipogundua kwamba kijana huyo wanayemtafuta ni mtu hatari sana. 

Polisi hao waliamini hilo jambo baada kuona nyumba nyingi zimeunguzwa kuachilia mbali hiyo iliyounguzwa usiku wa jana huku wao wakiwa humo humo kijijini. Hivyo waliendelea na kazi yao wakizunguka huku na kule huku wakishirikiana na mwanakijiji mmoja ambaye alijitolea kuwatembeza polisi hao akiwapeleka maeneo ambayo Zabroni hupenda kukaa. Walitembea kila sehemu lakini hadi jua linazama kamwe hawakuweza kumuona,ila kesho yake asubuhi hivyo hivyo harakati ziliendelea. 

Kama ilivyo ada walizulura kila kona kuanzia asubuhi mpaka jua la saa saba mchana,bado hawakuweza kumuona. Jioni ilipofika,polisi hao wakiwa tayari wamekata tamaa walirudi sasa kwenye gari yao ili wakapumzike. Ghafla mwanakijiji walio kuwa nae alimuona Zabroni akiwa juu ya tanuru akipangua matofali,mwanakijiji huyo alistuka akasimama kisha akasema kwa sauti ya chini. 

"Haya sasa mtu mwenye yuleee", alisema huku akinyoosha kidole chake kuelekea kule alipo Zabroni ambaye alionekana kuwa bize kupangua matofali kwenye tanuru la mzee Maguso,mzee ambaye anamkubali sana katika maisha yake. Kwa maana hiyo baadhi ya shughuli mbali mbali alikuwa akimsaidia,lakini pia kilichokuwa kikimfanya Zabroni ampende huyo mzee ni pale alipokuwa akimtia moyo na ujasiri katika mambo yake ya kulipa kisasi.

Jeshi hilo baada kumuona mtuhumiwa,hawakutaka kuamini mapema. Hivyo walichukuwa picha waliyokuwa nayo wakaitazama kisha wakamtazama na Zabroni kule alipo,ingawa alikuwa ameinamisha uso wake lakini kuna baadhi ya vitu walivitazama wakaamini kuwa ni yeye. Hapo ndipo waliposogea mpaka kwenye tanuru,kwa amri wakamtaka Zabroni ashuke kutoka juu ya tanuru. Zabroni aligoma alisema 

"Sishuki,kwani nyinyi akina nani? Na mnataka nini?.." majibu ya Zabroni yaliwastua polisi hao,mmoja akasema kwa sauti kali "Alo kwahiyo unapingana na serikali? Shuka haraka sana ..", alisema polisi huyo huku akimnyooshea bastora Zabroni. Lakini bado Zabro alionyesha kutostuka,kwa ujasiri alijibu "Sishuki mkitaka fanyeni jambo lolote,siogopi. Kwani serikali ndio nini? Achanani na mimi bwana", 

Zabroni alipokwisha kujibu hivyo aliendelea na kazi yake ya kupangua matofali wakati huo polisi nao wakizikoki bastora zao ili wamshuti kwa kigezo cha kukaidi matakwa yake,punde si punde polisi hao walifyatua risasi kama njugu lakini cha ajabu zilipomkuta Zabroni alicheka huku damu zikibubujika mwilini mwake kisha akapotea pale kwenye tanuru zikabaki nguo na vumbi huku mwenye mtukutu akiwa ameshayeyuka. Polisi hoi kila mmoja alikimbia anapo pajua yeye,ilimradi wafike kwenye gari lao. Lakini pia cha ajabu walipofika kwenye gari lao walimkuta mzee wa makamo akiwa na mkongojo wake kando kando ya gari hilo .

Jeshi lile la polisi walitaharuki kumuona yule mzee,ghafla waliingiwa na hofu huku kila mmoja akisita kulisogelea gari. Wakati huo upande wa pili alionekana polisi mwingine akija hea hea kwa kasi ya ajabu,alipolifikia gari alifungua mlango kisha akaliwasha. Kabla hajaondoka aliwatazama wenzake kisha akasema kwa sauti kuu "Mnashangaa nini? Hebu pandeni juu tuondoke ebo ", alisema hivyo huyo kamanda huku akivutia resi kiasi kwamba ilifanya gari hilo ya polisi kutoa mlio mkali. 

Makamanda nao baada kuambiwa kuwa wapande gari waondoke,walimtazama kwanza yule mzee waliomkuta pembeni ya gari lao kisha haraka sana walidandia ambapo kamanda yule aliyeshikiria usukani akaliendesha gari kulikimbia balaa la Zabroni. Baaada kutoweka, ghafla yule mzee aligeuka kutoka katika hali hiyo akawa mwenye Zabroni.

"Ahahahah", Zabroni aliangua kicheko kisha akasema "Mimi ni Zabroni", sauti hiyo ilijirudia mara mbili mbili.

Upesi akanuia maneno yake ili apate kupopetea maeneo hayo. Lakini kabla hajapotea, mara ghafla kijana Madebe alitokea akamshika bega kisha akamuuliza "Kwanini unauwa raia hovyo? Wanamakosa gani?.." Zabroni aliposikia sauti hiyo iliyoambatana na kuguswa kwake bega,aligeuka akamtazama mtu aliyemshika kisha akahoji "Hii ngoma ya kikabila hupaswi mrusi ama mzungu kutii maguu, kwani wewe unaniuliza kama nani labda" alihoji Zabroni huku akiwa amekunja uso wake. "Mimi Madebe, mtetezi wa wanyonge" alijibu Madebe.

"Ala! Kwahiyo umeamua kujitolea kwa ajili ya watu wa kijiji hiki?.." Zabroni alirudia kumuuliza Madebe,lakini Madebe hakujibu. Zaidi alinyoosha mkono wa kulia juu,punde si punde kwenye kiganja cha mkono ulitokea upanga. Panga ambalo lilimelemeta sana huku likionyesha makali yasiyo na mfano. Zabroni alistuka haraka sana alipotea akaibukia sehemu nyingine tofauti na ile ya awali,hapo sasa naye aliinyoosha mkono juu ila abadani hakikutokea kitu chochote. 

Hofu ilimjaa akajiuliza "Nifanye nini sasa ili nimkabili huyu mtu anaye taka kuharibu mipango yangu? ", wakati anajiuliza swali hilo,Madebe alitokea mbele yake akiwa na panga lake. alimtazama Zabroni kisha akasema"Wewe si mwanaume? Mbona sasa unanikimbia?", aliongea kwa kujiamini kijana Madebe huku akimsogelea Zabroni ilihari Zabroni naye akirudi nyuma. Mwishowe Zabroni aliamua kujibadilisha akawa katika umbile la nyoka aina ya cobra,hapo sasa ndipo ugomvi ulipo anza. 

Madebe alijitahidi kurusha panga lake kwa umahiri ili akate kichwa cha huyo nyoka, pia Zabroni naye ambaye yupo katika umbile la nyoka alifanya juu chini ili amgonge Madebe amtie sumu kali aliyokuwa nayo. Na alipoona hilo zoezi linakuwa ngumu,ndipo aliporusha mate lakini nayo hayakuthubutu kufua dafu kwa Madebe. Hakika ilikuwa vurugu maeneo hayo,ndege na wadudu mwitu walitulia kuona ugomvi huo wa aina yake.

Na wakati hayo yanajili kati ya Zabroni na Madebe,upande wa pili mzee Fungafunga alipata taarifa kuwa dada yake anamtaka Tina aende Dar es salam kuishi naye kwa maana kamkumbuka sana. 

Hivyo nafasi hiyo mzee Fungafunga aliitumia kama moja ya kuyatenganisha mahusiano ya mwanaye na kijana Zabroni. Alisubiri baadaye muda wa chakula cha usiku aseme na binti yake kuhusu taarifa hiyo ilihari moyoni akijisemea kwamba "Iwe isiwe lazima ataenda tu,sitaki mimi nipate mkwe katili kama huyu" alijisemea mzee Fungafunga huku kwingineko ugomvi ulikuwa bado unaendelea ila mwishowe Zabroni alipotea akaibukia juu kabisa ya kile cha mlima. Alisimama huko wakati huo akihema kwa nguvu ya ajabu akionekana kuchoshwa na balaa la mtukutuku mwenzie ambaye si mwingine ni Madebe. 

Hofu sasa ilianza kumtanda Zabroni, alijiuliza "Ni dawa gani anatumia huyu mtu?..", kabla hajapata jibu ,Madebe akatokea kwa mara nyingine tena. Safari hiyo alikuwa na sime mkononi yenye chata ya fuvu. Madebe akasema "Zabroni ulipo lala wewe ndipo tulipo amkia,nafikiri umefika wakati wako wa mwisho. 

Damu nyingi umemwaga lakini leo hii zitamwagika zako" alisema Madebe huku macho yake yakionekana kutisha yalifanana na macho ya nyoka,hali ambayo ilizidi kumtisha Zabroni. Aliogopa sana ila hakuwa na budi kupiga moyo konde ili amalizane na Madebe. 

Mvua ikaanza kunyesha,radi pamoja na ngurumo mbali mbali zililindima angani. Wakati huo huo Madebe akarusha sime yake,kabla haijamkuta mlengwa ambaye ni Zabroni. Zabro alilala,sime ikapita juu kisha papo hapo akajiugeuza akawa katika hali yake ile ile ya nyoka. Hakuwa na njia nyingine kwani kwa kasi aliyokuwa anatumia Madebe, ilimbidi Zabroni kutumia njia hiyo. Kweli juhudi yake hiyo iliweza kuzaa matunda,kwani alifanikiwa kumgonga Madebe mguuni baada Madebe kuzubaa kwa sekunde kadhaa. 

Madebe alianguka chini lakini pia kabla Zabroni hajafanya jambo lingine lolote juu yake,ghafla ile sime aliyoirusha ilirejea mkononi mwake ambapo bila kuchelewa aliitupa kwa Zabroni ambaye yupo katika umbile la nyoka,nayo ilimpata ubavuni hali ambayo ilimfanya arudi kwenye hali ya kawaida ambapo napo hakupoteza muda alipotea kisha Madebe naye akatoweka.

INAENDELEA

Powered by Blogger.