KARIBU USOME HADITHI NZURI ZA KUSISIMUA

Simulizi : Ndoa Yangu Inanitesa Sehemu Ya Saba (7)

simulizi nzuri ya maisha, ndoa yangu inanitesa
Kesho yake ilikuwa siku ya mimi kupimwa afya ikiwemo na kupimwa virusi vya Ukimwi, sikuwa na wasiwasi nilisubiri waje kunipima kwani nilijiamini sikuwa na virusi, japo nilifanya mapenzi na Jennifer kule Thailand bila kutumia kinga yoyote.Na hata mapenzi niliyofanya yenyewe yalimfurahisha na kumridhisha Jennifer na kukiri mimi ni miongoni mwa wanaume wanaojua mapenzi. Sikupenda Jennifer anidharau kwa upande wa kutomridhisha kimapenzi.

Waliingia Daktari waliovaa magwanda meupe wakiwa na vipimo vyao. Waliongozana moja kwa moja ofisini kwangu, cha ajabu baada ya kusalimiana nao walitaka nivue nguo nibaki na kaptula, jambo hilo nilipinga.

“Kama kunipima damu ninatolewa damu kwenye mkono sio karibu na uume wangu. Nyie ni daktari kweli?”

“Ndio sisi ni daktari unataka vitambulisho?”.

“Sina shida na vitambulisho vyenu. Nyie chukueni damu mkaipime, mkileta majibu mabaya nitarudia hospitali nyingine niliwaeleza waziwazi bila kuwaficha kitu.”Nikiwa nimeketi kitini,wao walikuwa wamesimama.

Haraka haraka daktari mmoja alitoa sindano iliyokuwa na kitu kama maji, sijui ilikuwa sumu au ilikuwa nini!. Maji hiyo ilikuwa ndani ya bomba la sindano. Kama cc 200. Sikuweza kuona nilikuwa nimegeuka kwa upande mwingine ili nisione sindano inavyopenya na kuingia kwenye nyama za mwili wangu. Kwa kifupi nilikuwa muoga wa sindano japo nilikuwa mtu mzima.

Wakati sindano ipo kwenye mshipa wa damu nilisikia kitu kama maji yenye uchungu wa dawa, nilipata maumivu makali nilipogeuka ndipo niliona akigandamiza bomba la sindano kwa haraka ili nisione kitu, lakini niliona kitu kilichoingizwa kwenye mshipa wa damu. Nilishindwa kujua kilikuwa ni kitu cha kuniletea matatizo ama kunijenga ndani ya mwili wangu.

“Dakitari wewe unanipiga sindano au umekuja kunitoa damu ili upime Virusi vya Ukimwi?. Iweje unipige sindano?”. Nilimuuliza daktari kwa hasira baada ya kusikia ile sindano mwili mzima, nilihisi kizunguzungu mwili ukakosa nguvu. Tofauti na kabla ya kuingiza sindano yao, halafu walikuwa bado hawajatoa damu.

“Usijali Sweedy sijakupiga sindano, nataka kutoa damu” alisema huku akivuta damu kwenye bomba la sindano. Na muda mfupi waliniaga, alionekana nesi mmoja kati ya wale waliokuja kunitoa damu mwenye majonzi. Alinitazama kama mtu aliyenionea huruma sana, machozi yalimlenga lenga lakini hakutaka niyaone aligeuka upande wa pili na kujifuta na kitambaa alichokuwa nacho mkononi. Nahisi alikuwa anajua kila kitu kilichotendeka kwa muda ule na sura yake ilikuwa sio ngeni machoni mwangu, lakini nilishindwa kumkumbuka vizuri. Alijua mipango yangu yote hasa ile ya kufunga pingu za maisha. Alijaribu kuwa wa mwisho kuniaga.

Nilisikia akiniambia “Pole sana Sweedy, moyo unaniuma Mungu akubariki maishani. Nenda kanywe maziwa mengi yatakusaidia”. Nesi huyo aliondoka taratibu, huku akigeuka nyuma na kunitazama kwa macho ya huruma. Nilishindwa kumjibu, nilibaki nikiyaganga maumivu ya sindano niliyochomwa mara ya kwanza, ambayo sikuweza kuielewa ilikuwa ya nini mwilini mwangu.

Robo saa baada ya wale daktari kuondoka mkono niliopigwa sindano na kutolewa damu nilihisi unakufa ganzi, kila nilipotafakari yale maneno ya yule nesi na kilio chake nilishindwa kumuelewa zaidi ya kujilaumu kwa nini nimekubali kupimwa pengine wamenipiga sindano yenye sumu ambayo itanidhuru. Kwa upande mwingine sikuamini niliona yule nesi alinipenda bure, na Mzee Jophu asingeweza kuwatuma watu wanipige sindano yenye sumu . Nilimuamini sana tajiri yangu.
Powered by Blogger.